Na: Calvin Gwabara
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii
imewataka Wananchi kwenye vijiji vinavyotekeleza Mradi wa Usimamizi shirikishi
wa Misitu ya Vijiji kuunga mkono kwa dhati jitihada za Mashirika ya TFCG na
MJUMITA kwa kukomesha kabisa vitendo vya uchomaji misitu ya vijiji ili waweze
kuendelea kunufaika na rasilimali hizo vizazi na vizazi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ally
Makoa wakati akizungumza na wananchi wa
kijiji cha Chabima wilayani Kilosa mkoani Morogoro wakati wa ziara ya kamati
hiyo ilipotembelea kujionea na kujifunza namna Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili
Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) wanavyotekeleza
Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) chini ya Mradi wa Kuleta
Mageuzi katika Matumizi ya Mkaa Tanzania (TTCS) inavyofanya kazi na kulinda
misitu huku ikinufaisha jamii.
“Tumeona kazi kubwa ya kutoa elimu ya utunzaji na usimamizi wa
misitu ya jamii iliyofanywa na wadau hawa lakini kiukweli bado kuna wimbi kubwa
sana la uchomaji wa misitu katika wilaya ya Kilosa kwenye njia ambayo tumepita
tukija kijijini kwenu, Miradi hii itakuwa na maana zaidi kama Wananchi
mtashiriki kikamilifu katika kuzuia mioto hii tuliyoiona njia nzima maana
inaharibu kabisa malengo ya Mradi na Serikali katika kutunza misitu hii muhimu
kwa ustawi wa Taifa letu”, alisema Mhe. Makoa.
Akielezea mbinu hiyo inavyofanya kazi huku akijibu baadhi ya
maswali ya Wabunge, Meneja wa Mradi huo Charles Leonard amesema mfumo huo unatekelezwa
baada ya Tafiti nyingi zilizofanywa kwenye nchi mbalimbali na kuonekana kufanya
vizuri nchini Zambia ambapo jamii zimeweza kutunza misitu baada ya kupata faida
kwa mtu binafsi,Vijiji na Serikali na tofauti na maeneo mengine ambayo jamii
inaona misitu ni mali ya Serikali tu.
Bw. Leonard amesema Mradi hauishii kwenye kutekeleza kwa
maneno tu bali una programu nzuri ya ufuatiliaji wa uchipuaji wa miti hiyo
kwenye vijiji vyote 41 ambayo inafanywa kwa kushirikiana na watafiti Kutoka
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Ndaki yake ya Misitu pamoja na
Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania TAFORI ambao hutoa mapendekezo na ushauri
wa namna bora ya utekelezaji na uboreshaji wa mfumo huo ingawa takwimu za mwaka
jana zimeonesha kuwa mfumo huo umefanya vizuri kwa zaidi ya asilimia 88.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG Bw. Charles Lyimo amesema Vijiji hivyo
havitaishia kunufaika na Mkaa, Mbao na Mazao mengine lakini pia vitaweza kupata
faida kwenye uuzaji wa Hewa ya Kaboni kwa kuwa miti mipya inayochipua itakuwa
na uwezo zaidi wa kuvuta hewa hiyo kuliko miti ya miaka mingi iliyozeeka.
Wakieleza namna walivyonufaika na Mradi huo Afisa Mtendaji wa Kijiji
kwa niaba ya Wananchi wa kijiji cha Chabima Bi. Marrygoleth Mlengeni amesema Mradi
ulianza mwaka 2017 lakini awali mwaka 2011 mradi wa MKUHUMI uliwezesha kutengeneza mpango wa matumizi bora ya ardhi
katika Kijiji chao kwa kupanga maeneo ya makazi,kilimo, misitu na ufugaji na
hivyo kusaidia katika usimamizi wa ardhi.
Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na
Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kwa pamoja wanatekeleza
Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) chini ya Mradi wa
kuleta Mageuzi katika ya Mkaa Tanzania (TTCS) kwa ufadhili wa Shirika la
Maendeleo la Uswiss (SDC).
0 Comments