Na: Farida Mkongwe - Morogoro.
Wanachama wa Mtandao wa Jamii wa
Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) wametakiwa kupaza sauti zao kukemea uharibifu wa mazingira na maamuzi yaliyo kinyume na taratibu za uhifadhi wa misitu yanayofanywa na baadhi ya viongozi na jamii nchini.
Afisa Misitu Mkuu kutoka Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Emmanuel Msofe wakati akifunga Warsha na Mkutano Mkuu wa 22 wa mwaka wa MJUMITA uliofanyika mjini Morogro. |
Wito huo umetolewa na Afisa
Misitu Mkuu kutoka Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bw.
Emmanuel Msofe wakati akifunga Warsha na Mkutano Mkuu wa 22 wa mwaka wa MJUMITA
uliofanyika kwa siku mbili Mkoani Morogro.
“Nyinyi Wanamtandao mmepata elimu
nzuri ya uhifadhi wa misitu ya Vijiji na Mazingira kwa muda mrefu mnajua Sheria
ya Misitu na Kanuni zake nendeni mkaelimishe na wengine kwenye maeneo mnayotoka
na mkapaze sauti zenu kwenye maeneo yote nchini pale mnapoona Sheria na Kanuni
hazifuatwi na jamii na viongozi katika uhifadhi wa Misitu na Mazingira”, alisisitiza Bw.
Msofe.
Amewataka kwenda kuzungumza
masuala ya uhifadhi kwenye mikutano yao mbalimbali ya vijiji na kutumia
mikutano hiyo katika kutoa elimu kwa jamii na watu wengine ambao hawana elimu
hiyo ili suala la usimamizi na uhifadhi wa misitu liwe la kila mwananchi na sio
wana Mtandao pekee.
Aidha Afisa Misitu huyo Mkuu amesema
pamoja na Elimu, Sheria na Kanuni za Misitu kuwepo lakini bado Tanzania
inapoteza kiasi cha hekta 460,000 Kila mwaka za misitu huku suala la moto
likiendelea kuchangia katika kuongeza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Mlezi wa MJUMITA Bw.
Charles Meshack amesisitiza fedha zinazopatikana kutokana na mazao ya misitu
katika vijiji irudishwe katika shughuli za uhifadhi wa misitu hiyo badala ya
kutumika kwenye mambo mengine wakati Kamati za Maliasili zikikosa vifaa vya
kufanyia kazi na jamii kukata tamaa kwa kukosa motisha.
Mlezi wa MJUMITA Bw. Charles Meshack akitoa neno wakati wa ufungaji wa Mkutano huo. |
Amesema idadi ya watu inaongezeka
kila mwaka lakini misitu na ardhi bado ni ileile hali inayopelekea uhitaji
mkubwa wa nishati na maeneo ya kuishi na kufugia na kuchangia katika migogoro
kati ya wakulima na wafugaji kwenye maeneo mengi nchini na hivyo kuwataka Wanamtandao
na jamii kutokaa kimya na kufumbia macho watu wanaoharibu misitu na mazingira
ili Dunia iendelee kuwa salama.
Afisa Misitu huyo Mkuu kutoka
Idara ya Misitu na Nyuki amesema ushindani wa matumizi ya maji baina ya
wanyama, binadamu na mimea ndio unaopelekea uhaba wa maji kwenye miji mingi kwa
sasa nchini hususani Dar Es Salaam na
hayo ndio matokeo ya mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na uharibifu wa
vyanzo vya maji na mazingira.
“Sote tunafahamu kuwa tukitimiza
wajibu wetu kila mmoja tunaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hivyo
tukarejeshe misitu yetu kupitia mfumo wa Kisiki hai na kuruhusu miti mingine
kukua na mbegu zilizo ardhini kuota lakini pia tupande miti kwenye maeneo
ambayo hayana miti kabisa kwa kufanya hivyo
tutaweza kuitunza misitu yetu na kufanya Tanzania kuwa kijani ifikapo mwaka
2030 kama ambavyo Mhe. Naibu Waziri wa Maliasili alivyotuagiza siku ya
ufunguzi”, alisisitiza Bw. Meshack.
Akitoa salamu za mkoa wa Morogoro
Afisa Maliasili wa Mkoa huo Bw. Joseph Chuwa amesema imefika wakati sasa mizani
ya ikolojia ya misitu na binadamu irejeshwe ili kunusuru Taifa kutoka katika
janga hili kubwa la Ukame na mabadiliko ya Tabianchi.
Afisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro Bw. Joseph Chuwa akitoa salamu za Mkoa wakati wa hitimisho la mkutano huo. |
“Sheria na Kanuni zilizopo
zitumieni kupaza sauti kwenye maeneo yenu na kuhakikisha kuwa zinatekelezeka
maana ninyi ndio mnaishi kwenye maeneo ya misitu na mnazungukwa na misitu kwa hiyo
msiruhusu majangili na watu wengine wasio na mapenzi mema na misitu kuiharibu mazingira na kuacha maeneo yenu yakiwa hayana miti”, aliongeza Bw. Chuwa.
WAJUMBE na WANAMTANDAO WA MJUMITA WAKIFUATILIA HOTUBA ZA UFUNGAJI WA MKUTANO HUO.
0 Comments