SUAMEDIA

SUA, RECODA na ADRA zaja na Mradi wa Kilimo na Masoko unaoweza kumpa mkulima uhakika wa chakula na masoko


Na Gerald Lwomile

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana  na Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya RECODA, ADRA Tanzania na ADRA Denmark, zimetekeleza mradi wa majaribio wa kuwajengea wakulima uwezo wa uzalishaji wenye tija na namna bora ya kuuza mazao yao. SUA kwa upande wake ilijikita zaidi katika kipengele cha utafiti ambao umeonesha kuwepo matokeo chanya na kuwa mifumo ya RIPAT na FMS kwa pamoja inamsaidia mkulima kuzalisha mazao bora na kuwa na uhakika wa masoko.

Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Kabote aliyekaa katikati akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa utafiti wa mradi wa Kilimo na Masoko, kulia ni Mkurugenzi wa ADRA-Tz Bw. Samwel Oyortey na kushoto waliokaa ni Dr. Dominick Ringo Mkurugenzi wa RECODA


Akizungumza Septemba 23, 2022 katika warsha ya siku moja ya kuwasilisha matokeo ya utafiti wa Mradi wa Kilimo na Masoko, Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Samwel Kabote amesema endapo mfumo huu utaendelea kufanya kazi kwa ufanisi basi utaleta mapinduzi makubwa katika kilimo na masoko nchini

 “Kwa upande wa utafiti mradi unatafiti juu ya uunganishwaji wa RIPAT (Rural Initiatives for Participatory Agricultural Transformation), yaani Jitihada Shirikishi za Kuleta Mageuzi ya Kilimo Vijijini, na FMS (Farmer Market School), yaani Shule ya Soko la Mkulima na matokeo yake kwenye kipato na uhakika wa chakula kwa wakulima wadogo” amesema Prof. Kabote

 Amesema mifumo hii miwili ya RIPAT na FMS iliyotumika kwenye mradi wa Kilimo Masoko itawajengea wakulima uwezo wa kuzalisha na kuuza mazao yao na matokeo yake ni kuongeza kipato na uhakika wa chakula kwa wakulima wadogo.

 Prof. Kabote amesema pia kuwa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la RECODA na SUA. Amesema [ia kwamba kupitia mradi huu wa Kilimo na Masoko, SUA imeweza pia kushirikiana na ADRA Tanzania na ADRA Denmark.

 Akitoa mrejesho wa utafiti huu, Mratibu wa mradi huo kwa upande wa SUA, Dkt. Emmanuel Malisa amesema ili kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wenye tija na upatikanaji wa masoko kunahitajika juhudi zaidi ya sasa ili kwenda mbali zaidi ya mashamba ya maonyesho na mafunzo katika ngazi za vikundi pekee. 

Wakulima wanafanya vizuri kwenye mashamba ya maonyesho na mafunzo katika vikundi lakini kwenye mashamba yao binafsi wapo ambao hawajaiga walichojifunza. Hivyo, bado juhudi zinahitajika zaidi.

 Dkt. Malisa amesema utafiti umeonyesha kuwa, kupitia mifumo hii miwili ya RIPAT na FMS, kuna uwezekano mkubwa wa mkulima mdogo kuboresha maisha yake, kuongeza kipato na kuwa na uhakika wa chakula.

Amesema wakulima waliokua katika vikundi vya kuweka na kukopa (VSLA) walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na mseto mkubwa wa chakula zaidi ikilinganishwa na wasio wanachama.

  “Wakulima waliotumia vyakula bora vya kulishia mifugo yao (mbuzi wa maziwa, kuku na nguruwe) walikuwa na nafasi ya 75% ya kupata chakula cha aina nyingi zaidi kuliko wenzao. Wakulima hawa waliongeza uwezekanno wa kupata nyama, mayai, na maziwa” amesema Dkt. Malisa.

  Aidha amesema matumizi ya chanjo ya kuku, mbegu bora, umwagiliaji ili kukabiliana na ukame na kuwa na mizunguko mingi ya uvunaji, na uuzaji wa mazao kwa pamoja kunaweza kumuinua mkulima kwa kiasi kikubwa.

 

Naye Mkurugenzi wa RECODA (Research, Community and Organizational Development Associates), Dkt. Dominick E. Ringo amesema mfumo wa RIPAT unatumika maeneo mengi nchini Tanzania, pamoja na nchi nyingine kama Kenya, Burundi, Rwanda na Nicaragua, na umeonesha mafanikio katika kuziba pengo la teknolojia za kilimo.

 Kwa upande ADRA Tanzania, Mkurugenzi wa shirika hilo, Bw. Samuel Oyortey alisema mfumo wa FMS umefanya vizuri Malawi, Zimbabwe na Uganda, na sasa kupitia mradi wa Kilimo na Masoko unafanyiwa majaribio Tanzania.

Dkt. Emmanuel Malisa aliyesimama akizungumza kabla ya kuanza kutoa mrejesho wa utafiti wa majaribio wa mradi wa Kilimo na Masoko


Post a Comment

0 Comments