SUAMEDIA

Waliohesabiwa Tanzania kufikia asilimia 99.93

 

Na: Sharon Sauwa

Dodoma.

 Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) imesema watu waliohesabiwa wamefikia asilimia 99.93 na waliobakia ni asilimia 0.07 ya kaya zote nchini hadi kufikia leo asubuhi.



 Akizungumza leo Jumatano, Agosti 31, 2022 Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema asilimia 0.07 ya kaya zilizobakia zitandelea kuhesabiwa hadi Septemba 5, 2022.

 “Simu zilizotolewa zitatumika kuwafikia ambao hawajahesabiwa kwa kuwa utaratibu maalum ulishaandaliwa namna ya kuzifikia kaya hizo kupitia viongozi wa mitaa na vitongoji,”alisema.

 Kwa upande wa sensa ya majengo, Dk Chuwa alisema hadi leo asubuhi jumla ya majengo 6,351,927 yalikuwa yameshahesabiwa ambapo taarifa za umiliki, mahali yalipo na taarifa nyingine zilizoainishwa katika dodoso la majengo zimekusanywa.

 Amesema makadirio ya operesheni anwani za makazi wanategemea kufikia majengo milioni 12.7 kwa nchi nzima.

 “Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ni Sh400 bilioni sawa na wastani wa Sh6, 265 au Dola za Marekani 2.7 kwa mtu mmoja,” amesema Dk Chuwa.

 Amesema misaada kutoka kwa wadau wa nje ya nchi ilikuwa ni kuwajengea uwezo wataalam na vishikwambi.

 Amefafanua kuwa msaada wa kuwajengea uwezo wataalam ulitolewa na nchi ya Marekani wakati vishikwambi vilitolewa na Korea Kusini, Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women).

 Aidha, amesema mkataba wa ajira za muda kwa ajili ya kazi za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 baina ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na makarani au wasimamizi wa sensa ambao ulianza Agosti 21, 2022 hadi Septemba Mosi, 2022 haujabadilika.

 “Kuanzia Septemba 2 hadi 5, 2022 iwapo kuna mtu ambaye atakuwa hajahesabiwa au majengo ambayo yatakuwa hayajahesabiwa. Mwananchi au mtu huyo anatakiwa kuwasiliana na viongozi wake wa Serikali na mitaa au kitongoji au kupiga simu kwa namba ambazo zimetolewa ili utaratibu wa kukusanya taarifa ufanyike,” amesema Dk Chuwa.

Post a Comment

0 Comments