Na Mwandishi wetu, Arusha
Vijiji 20 kati ya 49 Wilayani Longido, Mkoa wa Arusha,
vimetenga eneo la hekta 186.794.2 kwa ajili ya nyanda za malisho ili
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Katika wilaya hii, asilimia 95 ya wakazi ni wafugaji ambao
wanamiliki mifugo 918,248 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 hata hivyo hivi
sasa wamekosa malisho ya mifugo na maji kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Afisa mifugo na uvuvi wilaya ya Longido, Nestory Daqarro
akizungumza na waandishi wa habari za mazingira kupitia mradi wa uhifadhi wa
mazingira kwa maarifa asilia ambao unafadhiliwa na shirika la maendeleo la
umoja wa mataifa (UNDP) kupitia programu ya miradi midogo amesema wilaya hiyo,
imeathirika sana na mabadiliko ya tabia nchi.
Daqarro amesema kutokana na uhaba wa malisho ya mifugo na maji
katika wilaya hiyo, hivi sasa wafugaji wamehamia maeneo ya nje ya wilaya hiyo
kusaka malisho hivyo ili kukabiliana na changamoto hiyo wameamua kutenga maeneo
ya nyanda za malisho ambapo watapanda majani na kuweka maji.
"Serikali inatambua changamoto za wilaya kwani kwa mwaka
wa pili sasa hakuna mvua za kutosha hivyo, vijiji vimetenga maeneo ya nyanda za
malisho ambayo yataidhinishwa na serikali kuu ili kuokoa mifugo yao,"
amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Kimokowa Wilaya ya Longido, Kilel
Olenyokie Mollel amesema wameamua kutenga maeneo ya nyanda za malisho ili
kuyatunza kwa ajili ya ufugaji.
"Tumekuwa tukikabiliwa na ukame katika wilaya yetu hivyo
tumeona ni vizuri kutenga maeneo ya malisho ambayo hayatavamiwa," amesema.
Mwenyekiti Kijiji Cha Olbomba Kashira Alais amesema wamekuwa
wakitumia maarifa ya asili katika uhifadhi hata hivyo wanataka serikali
kutambua maarifa hayo ili kupunguza migogoro.
Masono Ole Malendai amesema wanawake wamekuwa waathirika
wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi lakini wanaamini suluhu ni matumizi ya
maarifa asilia.
Mradi wa uhifadhi mazingira kwa maarifa asilia unatekelezwa na
shirika la wanahabari la kusaidia jamii za pembezoni la MAIPAC kwa kishirikiana
na CILAO na unataratibiwa na Jumuiko la maliasili Tanzania (TNRF).
0 Comments