NA:Winfrida Nicolaus
Jamii imetakiwa kupata Elimu
ya Ufugaji wa Kuku kitaalam ili waweze kufuata taratibu zote za ufugaji ikiwemo
kuwapatia kuku chanjo na kuwatengea mahali sahihi pa kufugia kwa uzalishaji
wenye tija kwaajili ya kujikwamua kiuchumi.
Amebainisha hayo Afisa
Mifugo Mwandamizi Bi. Enesa Raphael Mlay kutoka Idara ya Tiba ya Mifugo na Afya
ya Jamii Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wakati akizungumza mubashara
kupitia SUA Radio kutoka katika Viwanja vya Maonesho ya 29 ya Wakulima,
Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki.
Amesema ni vyema jamii
ikapata elimu ya kuwatunza kuku kwa uzalishaji wenye tija hivyo Idara hiyo ipo
kwenye maonesho hayo ya wakulima kwaajili ya kutoa elimu kuanzia namna bora ya utunzaji
wa mayai kwaajili ya uzalishaji, utunzaji wa kuku kulingana na aina ya kuku na
umri, namna bora ya kuweka kuku wako kwenye banda pamoja na jinsi ya kuwapatia
chanjo kwaajili ya kuwaepusha na magonjwa.
Bi. Enesa Mlay amesema
uzalishaji wa kuku unaanzia kwenye namna bora ya utunzaji wa mayai ambapo mayai
hayo yanatakiwa kuhifadhiwa kwenye kasha kavu au mchanga ambao umekauka vizuri
ama mfugaji anaweza akatumia nguo chakavu kwaajili ya kutunzia mayai vilevile
kutokana na yai kuwa na pande mbili iliyochongoka na pana ni vyema ile
iliyochongoka kukaa chini na pana juu kwakuwa sehemu pana ndio inayopumua.
“Mwananchi anapotembelea
banda la SUA atakutana na kuku aina mbalimbali, atajifunza namna sahihi ya
kuwatunza, kuwaepusha na magonjwa vilevile jinsi ya kuwapatia chanjo hatua kwa
hatua kwa uzalishaji wenye Tija hivyo katika kuwatunza atakutana na Banda la
Mfano kwaajili ya kutunzia kuku ambalo limetengewa sehemu tatu kulingana na
umri wa kuku na kwa manufaa ya uzalishaji bora na wa tija” , amesema Bi. Mlay
Aidha amesema kuku
wanatakiwa kukaa kwenye umri tofauti kati ya Vifaranga na Mama zao, Majogoo,
Matetea na wale ambao wanalalia au wanataga na sehemu nyingine iwe kwaajili ya
wale wagonjwa ambapo mlango wake unatakiwa kuwa wa kujitegemea kwaajili ya
kuepuka kusambaza vimelea kwa kuku wengine hivyo SUA imekuwa na Banda la Mfano
kwaajili ya utunzaji wa kuku.


0 Comments