SUAMEDIA

Jamii imetakiwa kupata Elimu ya Ufugaji wa Kuku kitaalam ili waweze kufuata taratibu za ufugaji ikiwemo kuwapatia kuku chanjo

 NA:Winfrida Nicolaus

Jamii imetakiwa kupata Elimu ya Ufugaji wa Kuku kitaalam ili waweze kufuata taratibu zote za ufugaji ikiwemo kuwapatia kuku chanjo na kuwatengea mahali sahihi pa kufugia kwa uzalishaji wenye tija kwaajili ya kujikwamua kiuchumi.





Amebainisha hayo Afisa Mifugo Mwandamizi Bi. Enesa Raphael Mlay kutoka Idara ya Tiba ya Mifugo na Afya ya Jamii Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wakati akizungumza mubashara kupitia SUA Radio kutoka katika Viwanja vya Maonesho ya 29 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki.

Amesema ni vyema jamii ikapata elimu ya kuwatunza kuku kwa uzalishaji wenye tija hivyo Idara hiyo ipo kwenye maonesho hayo ya wakulima kwaajili ya kutoa elimu kuanzia namna bora ya utunzaji wa mayai kwaajili ya uzalishaji, utunzaji wa kuku kulingana na aina ya kuku na umri, namna bora ya kuweka kuku wako kwenye banda pamoja na jinsi ya kuwapatia chanjo kwaajili ya kuwaepusha na magonjwa.

Bi. Enesa Mlay amesema uzalishaji wa kuku unaanzia kwenye namna bora ya utunzaji wa mayai ambapo mayai hayo yanatakiwa kuhifadhiwa kwenye kasha kavu au mchanga ambao umekauka vizuri ama mfugaji anaweza akatumia nguo chakavu kwaajili ya kutunzia mayai vilevile kutokana na yai kuwa na pande mbili iliyochongoka na pana ni vyema ile iliyochongoka kukaa chini na pana juu kwakuwa sehemu pana ndio inayopumua.

“Mwananchi anapotembelea banda la SUA atakutana na kuku aina mbalimbali, atajifunza namna sahihi ya kuwatunza, kuwaepusha na magonjwa vilevile jinsi ya kuwapatia chanjo hatua kwa hatua kwa uzalishaji wenye Tija hivyo katika kuwatunza atakutana na Banda la Mfano kwaajili ya kutunzia kuku ambalo limetengewa sehemu tatu kulingana na umri wa kuku na kwa manufaa ya uzalishaji bora na wa tija” , amesema Bi. Mlay

Aidha amesema kuku wanatakiwa kukaa kwenye umri tofauti kati ya Vifaranga na Mama zao, Majogoo, Matetea na wale ambao wanalalia au wanataga na sehemu nyingine iwe kwaajili ya wale wagonjwa ambapo mlango wake unatakiwa kuwa wa kujitegemea kwaajili ya kuepuka kusambaza vimelea kwa kuku wengine hivyo SUA imekuwa na Banda la Mfano kwaajili ya utunzaji wa kuku.

 


Post a Comment

0 Comments