Na Nicholas Roman
Imeelezwa kuwa ugonjwa wa Kideli au Mdondo ambao husababishwa
na virusi ni miongoni mwa magonjwa hatari ambayo huambukizwa kwa ndege kwa kasi
kubwa na kusababisha vifo hasa ndege aina ya kuku ambao ndio huathirika zaidi
Hayo yamesemwa na Mhadhiri toka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya ya Binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. James Mushi wakati akizungumza na SUAMEDIA
Dr. Mushi amesema ugonjwa husambazwa haraka toka kuku mmoja
kwenda kwa mwingine kupitia kinyesi au ute wa ndege aliyeambukizwa, na pia
virusi hivi vinaweza kuenezwa kupitia vyombo, chakula, watu, hewa au hata ndege
wa porini wenye virusi vya ugonjwa huo.
Amesema ugonjwa huo mara nyingi huwa unaathiri zaidi maeneo
ya mfumo wa hewa, mfumo wa chakula pamoja na mfumo wa fahamu ambapo maeneo hayo
yanapoathirika humpelekea kuku kufikia kwenye hatua ya mwisho kabisa kuonekana
kama aliyechanganyikiwa na hatimae kifo
‘‘Ugonjwa huu unapoingia huwa na awamu kadhaa na awamu ya
kwanza unaweza usione dalili zozote lakini unaona tu kuku wanakufa kwa wingi
kwenye banda na inawezekana ukawamaliza mpaka asilimia tisini (90%”, Amesema
Dkt. Mushi
Amesema dalili za ugonjwa huu ni hukohoa, kuhema kwa shida,
vifo vya ghafla,kutoa udenda mdomoni, kukosa hamu ya kula, kuharisha kinyesi
cheupe na kijani, kukakamaa viungo au kupooza hasa mabawa, shingo na miguu na
kupunguza utagaji
Ameongeza kuwa kwa kawaida magonjwa ya virusi hayana tiba
hivyo njia pekee ambayo inaweza kumsaidia mkulima au mfugaji ni chanjo ambayo
itamsaidia kuku au ndege wake asipate na ugonjwa huo na hata magonjwa mengine.
Ametaja njia nyingine ya kuwasaidia kuku waliobaki ni kuwahamisha kuku wote ndani ya banda na kuliacha banda hilo kwa muda usiopungua wiki tatu huku ukilipulizia dawa na baada ya kufanya utaratibu huo pale utakapowarejesha kuku waliosalia au kuku wengine wapya ni muhimu kufuwata utaratibu ili kulinda usalama wa kuku na ndege kwa kuwachanja.
0 Comments