SUAMEDIA

SUA imesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yatatatua changamoto za kilimo nchini

 

Na Gerald Lwomile

SUA

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema endapo kutakuwa na matumizi endelevu ya Teknolojia ya Mawasiliano nchini yasiyo na vikwazo basi Kilimo cha nchi hii kinaweza kukua kwa kasi na kuwa na tija kwa mkulima binafsi na Taifa kwa ujumla.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Georgia cha nchini Marekani Prof. Glen Rains katikati akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mradi wa SUA YEESI Lab, aliyesimama katikati mwenye Kaunda Suti ni Dkt. Kadeghe Fue Mkuu wa Mradi

Hayo yamesemwa na Prof. Wulystan Mtega kutoka SUA wakati akitoa salaamu kwa niaba ya Mkuu wa Kampasi ya Solomon Mahlangu katika ufunguzi wa Mhadhara wa siku mbili unaofanywa na Mradi wa ‘SUA YEESI Lab’ unaowawezesha vijana kutumia akili bandia katika kuangalia changamoto mbalimbali katika kilimo.

Prof. Mtega amesema hivi sasa namba ya Wataalamu ni ndogo katika kuwafikia wakulima nchini hivyo utumiaji wa Teknolojia ya Mawasiliano unaweza kuja na aina ya mawasiliano ‘App’ inayoweza kutatua changamoto mbalimbali katika kilimo kwa upatikanaji wa taarifa sahihi na muhimu kwa wakati.

Naye Mkuu wa Mradi huo Dkt. Kadeghe Fue ambaye pia ni Mhadhiri SUA amesema Mradi huo umelenga kuwajengea uwezo vijana katika kuhakikisha wanakuwa na matumizi sahihi ya Teknolojia ya Mawasiliano na Habari na hasa kwenye kilimo ili kutatua changamoto zinazowakabili wakulima.

http://suamedia1994.blogspot.com/2022/05/matumizi-ya-teknolojia-ya-mawasiliano.html

Dkt. Fue amesema katika kutumia teknolojia hiyo ya akili bandia wanafunzi wanaweza kujifunza namna ya kuangalia changamoto katika kilimo kama magonjwa, magugu, namna mmea unavyoendelea shambani kwa kutumia vifaa kama Kompyuta, Kamera na vingine kama hivyo ili kuona tabia ya mmea katika makuzi yake.

Amesema kutokana na utaalamu watakaoupata vijana hao wanaweza kuanzisha Makampuni ambayo yatasaidia kuangalia na kupata taarifa sahihi zitakazosaidia kutatua changamoto lakini pia kuwa kichocheo cha mabadiliko katika namna ya kufanya kilimo chenye tija.

Amesema kuwa matumizi ya Teknolojia hizi yamerahisishwa kiasi mkulima anaweza kupiga picha au kutuma sauti kwa njia ya mtandao na kupata suluhisho la changamoto ya ugonjwa au kutokuwepo kwa maendeleo katika mmea wake.

Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Georgia cha nchini Marekani Prof. Glen Rains amesema kuwa tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya Dunia mwaka 1945, Dunia ikiwemo Marekani iliingia katika changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira na ndipo teknolojia za kisasa zikaanza kutumika ili kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya kilimo unaongezeka.


Washiriki wa Mradi wa SUA YEESI Lab wakisikiliza mawasilisho kutoka kwa Prof. Rains 

Amesema ni muhimu wakulima wakatumia teknolojia za kisasa ikiwemo Teknolojia ya Mawasiliana na Habari katika kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali katika sekta hiyo muhimu ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Ametolea mfano kuwa uzalishaji wa mazao ya Pamba umeongezeka maradufu kufuatia kuwepo kwa Teknolojia hizo za Mawasiliano kama  mtandao na kwa kutumia vifaa kama Mkongo, Kompyuta na Kamera changamoto nyingi zimetatuliwa na kuinua kilimo kwa kiasi kikubwa

Post a Comment

0 Comments