SUAMEDIA

Shanghai yaripoti vifo vya kwanza vya mlipuko wa sasa wa COVID-19

 



Mamlaka ya Shanghai imeripoti leo Jumatatu vifo vya kwanza vya ugonjwa wa COVID-19 katika mlipuko wa hivi karibuni katika mji huo wenye idadi kubwa ya watu na mji tajiri zaidi nchini China. 

Mkaguzi wa Tume ya Afya Wu Ganyu amewaambia waandishi wa habari kuwa watu wote watatu waliofariki walikuwa wazee, na walisumbuliwa na magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu na kwamba bado walikuwa hawajapokea chanjo dhidi ya virusi vya corona. 

Wakaazi wengi wa Shanghai yenye jumla ya watu milioni 25, wamekuwa chini ya vizuizi vikali kwa wiki ya tatu huku China ikiendelea na mkakati wake wa kukabiliana na kusambaa kwa Covid-19. 

Jiji hilo liliripoti maambukizi zaidi ya 300,000 mwishoni mwa mwezi Machi. 

Shanghai, mji wenye bandari kubwa ya China na muhimu zaidi kwa soko la hisa, umeonekana kutokuwa tayari kwa vizuizi hivyo ambapo wakaazi walikosa chakula na mahitaji muhimu ya kila siku huku wakistahimili vikwazo hivyo.

CREDIT MUUNGWANA

Post a Comment

0 Comments