SUAMEDIA

Megawati 200 Za Jotoardhi Kupatikana Kabla Ya 2025

 


SERIKALI imesema Tanzania itazalisha umeme wa megawati 200 unaotokana na jotoardhi kabla ya mwaka 2025.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba alisema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua vyanzo vya nishati ya Jotoardhi vya Kiejo-Mbaka na Ngozi mkoani Mbeya.


Alisema Tanzania kuna jumla ya maeneo 52 yanayoweza kutoa nishati ya jotoardhi ambayo tayari yameshatambuliwa.


Alisema kwa ujumla serikali ina mpango wa kuongeza megawati 1,100 zinazotokana na nishati jadidifu kabla ya mwaka 2025 na zitatokana na vyanzo mbalimbali kama vile jotoardhi, jua na upepo.


“Wizara ya Nishati inaweka nguvu kubwa katika kuendeleza vyanzo vya nishati ya jotoardhi kwa sababu vyanzo hivyo haviishi, hivyo ukaguzi uliofanywa katika maeneo hayo ya jotoardhi utasaidia serikali kuona hatua stahiki za kuchukua ili kuendeleza vyanzo hivyo.”


"Kipindi cha ukame maji yanaweza kupungua, lakini jotoardhi katika kipindi cha ukame au mvua, mvuke unaotoka chini ya ardhi uko palepale," alisema.


Alisema Kenya ina zaidi ya megawati 1,100 zinazotokana na jotoardhi na Tanzania kutokana na eneo lake kubwa kupitiwa na Bonde la Ufa kuna uwezekano wa kupata umeme mwingi zaidi unaotokana na nishati hiyo.


"Mfano hapa mkoani Mbeya katika eneo hili la Rungwe kumeonekana kuna uwezekano mkubwa wa kutoa nishati ya jotoardhi kwa sababu tawi moja la Bonde la Ufa limeingia katika eneo hili na jingine limeelekea upande wa Malawi," alieleza.


Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mathew Mwangomba alisema eneo la Kiejo-Mbaka linaweza kuzalisha megawati 60 zinazotokana na jotoardhi.


Alisema serikali imetoa Sh bilioni 20 kwa ajili ya uendelezaji wa eneo hilo na sasa wamenunua mtambo wa kuchoronga eneo hilo na kwamba wataalamu wa TGDC na wahisani wameshirikiana katika kufanya tafiti zote zinazotakiwa.


Alisema katika eneo la Ngozi, inategemewa kuwa litazalisha megawati 70 zinazotokana na jotoardhi na kwamba TGDC imejipanga vizuri katika kuhakikisha Tanzania inapata umeme kutoka kwenye nishati hiyo jadidifu.

Post a Comment

0 Comments