Na Editha Mloli
Jamii nchini imeaswa kuwatumia vema wataalamu wanaohitimu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kuwa wamebobea katika utaalamu wa aina mbalimbali ambao unaleta tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla na kuwasaidia kuondokana na ufanyaji kazi wa mazoea na kuepuka umaskini.
Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Shamba la Mafunzo Roman Mfinanga kutoka SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Mfinaga amesema wanafunzi baada ya kujifunza kwa vitendo wanapata mbinu na maarifa ya kuwasaidia wanajamii katika kuzalisha kwa kiwango kikubwa hata kama mkulima ana eneo dogo.
“Wanafunzi wetu baada ya kuhitimu hapa wataenda kufanya kazi katika maeneo mbalimbali kwa wananchi wetu na kule katika kuwahudumia wananchi wanaweza kutumia zile mbinu na maarifa ambayo wameyapata hapa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuzalisha kwa kiwango kikubwa kwa kuwa wanatumia njia za kisasa zaidi”, amesema Mfinanga.
Aidha Mfinanga amewataka wanafunzi kuwa na bidii katika kuyatumia vizuri mafunzo wanayoyapata kutoka SUA ili kuweza kupata maarifa mengi baada ya kuhitimu chuo na kuweza kujiajiri wenyewe lakini pia kuisaidia jamii kuzalisha kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wao wanafunzi ambao wapo katika mafunzo hayo wamesema wananufaika vizuri kutokana na mafunzo wanayoyafanya kwa vitendo kulingana na kile walichojifunza darasani kwani kinawasaidia kupunguza gharama za kwenda mbali kuyapata mafunzo hayo.
Wanafunzi hao pia wamewaasa vijana wenzao kupenda kujishughulisha na kilimo kwa kuwa ndio uti wa mgongo wa Taifa na kilimo hicho kitawasaidia vijana kujiajiri wenyewe bila kutegemea ajira kutoka serikalini.
0 Comments