SUAMEDIA

Dkt. Innocent Babili: Vijana wachague Chuo cha SUA kwa ajili ya kupata mafunzo mbalimabali yatakayo wawezesha kujiajiri kupitia kilimo biashara

 Na Hadija Zahoro na Adam Maruma    

 Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza ICE ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA imewataka vijana wakichague Chuo cha SUA kwa ajili ya kupata mafunzo mbalimabali yatakayo wawezesha kujiajiri kupitia kilimo biashara.

Mkuu wa Kitengo cha Ugani ICE Dkt. Innocent Babili akizungumza juu ya vijana wachague Chuo cha SUA kwa ajili ya kupata mafunzo mbalimabali yatakayo wawezesha kujiajiri kupitia kilimo biashara


Akizungumza mubashara na SUA Redio kupitia Kipindi cha Kapu la Leo, Machi 22 mwaka huu Mkuu wa Kitengo cha Ugani ICE Dkt. Innocent Babili amesema SUA kupitia Taasisi hiyo ina kozi mbalimbali za muda mrefu pamoja na muda mfupi ambazo zitawasaidia vijana kuacha kulalamikia suala la ukosefu wa ajira nchini.


‘‘Sisi Tunawahamasisha na kuwatia moyo vijana kwamba wachague  SUA kwa kozi za aina mbalimbali ziwe za muda mfupi au muda mrefu akishamaliza SUA tayari anaweza kufanya shughuli zake mwenyewe’’, amesema Dkt. Babili.


Awali, Dkt. Babili amesema kuwa kwa wadau watakaojiunga kozi ya muda mrefu, eneo la vitendo litaongezwa kwa lengo la kuwaongezea ujuzi  zaidi na kwamba unaweza kuwapata wahusika wa ICE  kwa kuwatembelea moja kwa moja Chuoni hapo au   kupitia  tovuti  yao ya www.ice.sua.ac.tz.


Aidha, Dkt. Babili amesema wao kama ICE wanaona fahari kuona uongozi wa Chuo, Taasisi za aina mbalimbali pamoja na Serikali za Mitaa ikiwemo za Manispaa ya Morogoro, Wafadhili, Maafisa wa kilimo wa manispaa ya Mororgoro pamoja na  Shirika la Chakula Duniani (FAO), wanaonesha ushirikiano  kuhakikisha wanapata wadau mbalimbali wanaohitaji huduma zao.  

Ameongeza kuwa Taasisi hiyo haiwasaidii watu moja kwa moja kuhakikisha wanapata masoko badala yake inawaunganisha na vijana ambao wanafanya shughuli mbalimbali ikiwemo uoteshaji wa miche pamoja na ufugaji wa vifaranga vya samaki aina ya sato na kambare, ambao nao wamepata ujuzi kupitia ICE.

‘‘Hatusaidii watu moja kwa moja  kupata masoko lakini kama tukipigiwa simu sisi kama ICE kwamba wapi mtu anaweza kupata vifaranga vya samaki kwasababu SUA tunazalisha vifaranga vya sato na kambare hivyo tunawaunganisha na  vijana ambao wanafanya shughuli hizo’’.






Post a Comment

0 Comments