SUAMEDIA

Vijana 1500 wamepata mafunzo ya Kilimo cha Mbogamboga kibiashara kupitia Kitalu Nyumba ili kuweza kujiajiri wenyewe

 NA: Gojo Mohamed

Takribani vijana 1500 wamepata mafunzo ya kilimo cha mboga mboga kibiashara kupitia kitalu nyumba ambayo yatawasaidia katika kuongeza ujuzi na maarifa ili kuboresha uzalishaji wa mazao yenye tija pamoja na kuweza kujiajiri wenyewe.

Mafunzo hayo ya kilimo cha mboga mboga kibiashara kupitia kitalu nyumba yametolewa na Taasisi ya Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA (SUGECO) katika mikoa ya Singida  na Tabora chini ya Ufadhili wa Ofisi ya Waziri Mkuu SeraBungeKaziVijanaAjira na Wenye Ulemavu.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Jeshi Godfrey Lupembe  amewapongeza waratibu wa mafunzo hayo kwa kutoa elimu hiyo kwani ni muhimu sana kwa vijana hao na amesema kuwa kama Halmashauri wapo tayari kuendeleza na kujipanga na Mradi huo. 

‘‘Nipende kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuipa kipaumbele Sekta ya Kilimo katika kuhakikisha elimu ya kilimo inaweza kufika sehemu mbalimbali ikiwemo katika eneo letu sana sana katika suala la kuwahamasisha vijana kujikita kwenye kilimo na kuondokana na zana ya kuajiriwa tu kwani wanaweza kujiajiri pia kupitia kilimo ’’, amesema Jeshi Godfrey

Kwa upande wake Afisa Kilimo na Mratibu wa Kitalu Nyumba Halmashauri ya Nzega Mkoani Tabora Bw. Nickodemas Hando amesema wana matarajio makubwa sana kutokana na elimu hiyo ya kitalu nyumba kwa sababu wanahitaji kuzalisha mazao ya mboga mboga ya kutosha na yatakayowawezesha kulisha mpaka wilaya za jirani.

Naye Daniel Rwemamu mmoja wa wanufaika wa Mradi huo kutoka Halmashauri ya Nzega mkoani Tabora amesema amefurahishwa sana na mafunzo hayo ambayo yameendeshwa na SUGECO kw kuwa kupitia mafunzo hayo ameweza kujua ni kwa namna gani anaweza kulima kilimo biashara pamoja na kujua kanuni na taratibu za kilimo hicho. 

‘‘Naishukuru sana Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutupatia vijana elimu hiyo  lakini naiomba Serikali baada ya mafunzo hayo tuweze  kupatiwa vitendea kazi  ili tuweze kulima kwa ufanisi zaidi na kujipatia kipato na ujuzi wa kilimo biashara kupitia kitalu nyumba’’, amesema Daniel Rwemamu.








Post a Comment

0 Comments