SUAMEDIA

SUA kupitia Shule Kuu ya Elimu kuendelea kuzalisha Walimu wenye ubora katika Fani ya Sayansi

 

Na: Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Shule Kuu ya Elimu imeweka mkakati wa kuendelea kuzalisha walimu wenye ubora katika fani ya sayansi ili kuondokana na changamoto ya uhaba wa walimu wa Sayansi uliopo nchini.

Kaimu Naibu Amidi Shule Kuu ya Elimu SUA Dkt. Jamal Jumanne  akizungumzia mkakati wa kuendelea kuzalisha walimu wenye ubora katika fani ya sayansi ili kuondokana na changamoto ya uhaba wa walimu wa Sayansi

Hayo yameelezwa Machi 23, mwaka huu na Kaimu Naibu Amidi Shule Kuu ya Elimu SUA Dkt. Jamal Jumanne wakati akizungumza na SUAMEDIA kupitia SUAFM katika kipindi cha Mchakamchaka.

Dkt. Jumanne amesema kuwa SUA kama Taasisi ya kijamii iliyoamua kutenga jukumu pamoja na vyuo vingine katika kusaidia kuzalisha walimu itahakikisha inaandaa walimu wenye ubora wa kutosha hususani katika fani ya sayansi ambayo imeonekana kuwa na uhaba wa walimu.

“Tangu tumeanza uzalishaji wa walimu na sisi tunazalisha walimu wa sayansi, walimu hao tunaowazalisha wamekuwa walimu wanaokubalika sana kutokana na idadi inayochukuliwa kwenda kufundisha, tumejua hayo kutoka kwenye tafiti ndogondogo ambazo tunazifanya’’, amesema Dkt. Jumanne

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mitaala na Ufundishaji Shule Kuu ya Elimu SUA Dkt. Thabita Lupeja amesema mojawapo ya mikakati waliyonayo ni kubuni mbinu za kuweza kufundisha wanafunzi wanao waandaa, kuboresha ufundishaji wa masomo ya sayansi na hatimae kuweza kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia nchini.

Amesema watahakikisha Sayansi inayofundishwa inaenda sambamba na maisha halisi ili mwanafunzi aweze kuwa na shauku ya kusoma masomo ya sayansi.

“Maisha yote tunayoishi ni sayansi, unapopika chakula chako hiyo ni “chemical change” yaani badiliko la kikemikali na hiyo ni sayansi, unapofua pia ni sayansi lakini bado kuna baadhi ya watu wanaona ni ngumu kwahiyo katika kuhakikisha walimu tunaowaandaa wanakuja kuwa waalimu wazuri tunajaribu kutengeneza njia rahisi ya ufundishaji na yenye ubora kwa walimu hao tunaowaandaa’’, amesema Dkt. Lupeja.

                                      

Mkuu wa Idara ya Mitaala na Ufundishaji Shule Kuu ya Elimu SUA Dkt. Thabita Lupeja akizungumzia mikakati waliyonayo katika kubuni mbinu za kuweza kufundisha wanafunzi wanao waandaa, kuboresha ufundishaji wa masomo ya sayansi


KATIKA VIDEO 


 

Post a Comment

0 Comments