NA Editha Mloli
Mahusiano mazuri pamoja na Ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na wananchi wa Lushoto mkoani Tanga umekuwa sababu kubwa ya kuufanya msitu wa mafunzo wa Mazumbai kuendelea kubaki katikia katika uasili wake.
Hayo yamezungumzwa na Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanayamapori na Utalii Prof. Suzana Augustino wakati akizungumza na SUAMEDIA ambapo amesema tangu kuanzishwa kwa msitu huo wamekuwa wakishirikisha jamii katika kutunza na kulinda msitu huo wa asili wa Mazumbai.
Prof. Suzana amesema kuwa katika Msitu huo wa asili katika kuutunza na kuulinda wamekuwa wakitoa ajira za muda mfupi kwa wananchi wa maeneo hayo ambapo jambo hilo pia limekuwa chachu kwa wananchi kuendelea kulinda msitu huo ili wasipoteze ajira hizo za muda wanazozipata.
Katika suala zima la usimamizi wa msitu huo, Rasi huyo wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii amesema kuwa viongozi wa Serikali za vijiji wapo katika Kamati iliyoundwa na Chuo cha SUA ya usimamizi wa msitu huo kwa kuwa viongozi hao wanaishi na wananchi na wanaaminika kwa wananchi wao.
“Siri ya kuendelea kutunza Msitu wa Mazumbai ni yale mahusiano mazuri ambayo Chuo kupitia Ndaki imekuwa nayo na wale wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka msitu wa hifadhi wa Mazumbai na tangu kuanzishwa kwake msitu ule tumekuwa tunashirikisha jamii kwenye kutunza na kulinda kuna ambao wanapata ajira za muda mfupi kama vile walinzi”, amesema Prof. Suzana.
Akizungumzia utunzaji wa Msitu huo upande wa Serikali amesema Serikali ya wilaya imekuwa ikishirikiana vyema kwa kuwashirikisha katika vikao vyao vinavyohusu utunzaji wa mazingira pamoja na misitu.
Prof. ameongeza kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kutokata miti iliyopo katika msitu kwani Msitu huo wa Mazumbai umekuwa ukitunza vyanzo vya maji katika Kijiji cha Mgwashi hivyo wananchi wamekuwa wakitunza msitu huo ili kutopata adha ya maji.
Aidha amesema wamekuwa wakiwahamasisha sana wananchi kutunza miti ya asili katika maeneo yaliyozunguka Msitu wa Mazumbai pamoja na kupanda miti yao kwa ajili ya matumizi kama kuni na mbao ambayo itakuwa miti mbadala kuliko kuharibu miti ya asili.
0 Comments