Na: Amina Hezron
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Idara ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani imetenga Ekari takribani 220 kwa ajili ya uzalishaji wa Mbegu za Mahindi, Mpunga na Maharage ili kuchangia maendeleo ya kilimo nchini.
![]() |
| Mkuu wa Idara ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani Dkt. Kudra Abdul akizungumzia kuzalisha mbegu bora zitakazowafikia wakulima |
Akizungumza na SUAMEDIA Mkuu wa Idara ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani Dkt. Kudra Abdul amesema Chuo kimeamua kuzalisha mbegu bora zitakazowafikia wakulima hao ili kuwasaidia katika uzalishaji wa mazao kwa kuwa upatikanaji wa mbegu zenye ubora umekuwa ni changamoto kubwa kwa wakulima.
“Mikakati ilianza tangu mwaka 2019 ambapo tukatafuta kibali cha kuzalisha mbegu tukapata kutoka kwa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania TOSCI ambao ndiyo wanatoa vibali, bahati nzuri Chuo kina maeneo makubwa tu ya kuzalisha hivyo tumeshapatiwa shamba hilo ambapo mwaka huu tumeona tuanze na ekari 50 “, amesema Dkt. Kudra .
Dkt. Kudra ameeleza kuwa Chuo cha SUA kina wataalamu wa kutosha wa kuzalisha mbegu hivyo kwa sasa watazalisha kwa wingi mbegu hizo ili zikawasaidie wakulima.
“Katika upandaji wa mbegu mahindi tutapanda ekari 15, maharage ekari 5 na mpunga ekari 30 ambapo tunategemea kuzalisha mbegu tani 100 kwa kuanzia kwa mwaka huu”, amesema Dkt Kudra.
Mkuu wa Idara ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani amesema kuwa maandalizi ya upandaji wa mbegu hizo yameshaanza ambapo tayari uchimbaji wa mabwawa kwaajili ya upatikanaji wa maji kwaajili ya kumwagilia mashambani umeshafanyika na maji yameshaanza kuingia.

0 Comments