Na.Vedasto George.
Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA imeanza kutekeleza Miradi mitatu ya maji kwenye majimbo matatu ya Wilaya ya Morogoro ambapo hadi kukamilika kwake itagharimu zaidi ya shilingi Bilioni moja, Miradi ambayo inatajwa kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Mhandisi Grace Lyimo Meneja wa RUWASA wakati akizungumza na SUAMEDIA ofisini kwake juu ya umuhimu wa Maadhimisho ya Wiki ya Maji ambayo kilele chake ni Machi 22 kila mwaka.
Mhandisi Lyimo amesema kwa kutambua umuhimu wa rasilimali hiyo pamoja na changamoto wanazozipata wananchi ikiwemo ya kutembea umbali mrefu wakitafuta huduma hiyo muhimu ya maji tayari serikali kupita Mradi wa UVICO 19 imeidhinisha zaidi ya shilingi bilioni moja fedha ambayo itatumika kuboresha na kujenga miundombinu mipya ya maji.
Mhandisi huyo ameitaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Maji Mvuha ambao utahudumia vijiji vyote vya maeneo hayo, Mradi wa maji Kikundi ambao upo Morogoro Kusini Mashariki ambapo ujenzi wa kisima na tenki lenye ukubwa wa lita 150,000 unaendelea huku mradi mwingine ukiwa ni Mradi wa maji Kauzeni ambao unafanyiwa maboresho.
“Sisi RUWASA wilaya ya Morogoro tumepatiwa Miradi mitatu kwenye majimbo matatu ya wilaya ya Morogoro na Mradi mmoja upo jimbo la Morogoro Kusini ambao ni Mradi wa maji Mvuha pale tunaenda kuboresha huduma ya maji kutoa maji kwenye mto Mvuha kuyaingiza kwenye matenki na kuyasambaza kwenye vijiji vyote vya mvua lakini pia tuna miradi ya maji kwenye jimbo la Morogoro Kusini Mashariki pamoja na Mradi wa maji kwenye jimbo la Morogoro mjini pale Kauzeni na miradi yote hii hadi kukamilika kwake itatughalimu kiasi cha shilingi bilioni 1.6”, amesema Mhandisi Lyimo.
Aidha Mhandisi huyo amesema hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Halmashauri ya wilaya ya Morogoro inazidi kuimarika ambapo mpaka sasa watumiaji wa maji zaidi ya 260,000 tayari wamefikiwa ikiwa ni sawa na 69% ya wakazi wote huku akisema hadi kufikia mwaka 2025 serikali itakuwa imefikia vijiji vyote katika wilaya hiyo ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya maji.
Katika hatua nyingine Mhandisi Grace Lyimo amesema lengo la kuadhimisha wiki ya maji kila mwaka ni kuikumbusha jamii pamoja na wadau wa maji duniani kote kuendelea kulinda na kutunza vyanzo vya maji huku akisema Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini RUWASA imeadhimisha wiki ya maji tangu tarehe 16 mwezi huu wa tatu kwa kupanda miti kwenye vyanzo vya maji zaidi ya 200 huku kwenye kilele cha wiki ya maji wakiwa wamepanda miti 400 kwenye chanzo cha maji cha Mto Mbezi uliopo kwenye kijiji cha Tegetero Morogoro vijijini.
Nao baadhi ya wananchi akiwemo AIi Kapugwa na Mawazo Kaboge kwa pamoja wameishukuru serikali kwa kuanza kutekeleza miradi ya maji kwenye maeneo yao huku wakisema ujio wa miradi hiyo pia umesaidia kuwapatia ajira wao kama vijana wazawa wa vijiji hivyo.
Kwa upande wake Mhandisi Juma Mgaigwa anayeshughulikia Mipango na Usanifu wa Miradi RUWASA amesema miradi yote ya maji inayotekelezwa katika wilaya ya Morogoro kupitia Mradi wa UVICO 19 inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita huku Mhandisi JOSEPH PETRO msimamizi wa Mradi wa maji Kikundi kupitia kampuni ya Clalon Technology Company amewatoa wasiwasi wakazi wa kijiji cha Kikundi na kusema Mradi huo utakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na serikali.
.jpg)

.jpg)
.jpg)
0 Comments