SUAMEDIA

SUA kuchapisha matokeo ya Tafiti kwa Lugha rafiki kwa wakulima

 Na Editha Mloli

Katika kuwasaidia wakulima nchini pamoja na kuinua kilimo kupitia tafiti mbalimbali zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Chuo hicho kimesema kinachapisha matokeo ya tafiti hizo katika vijarida kwa lugha Rafiki kwa wakulima, japokuwa tafiti hizo zinafanyika kwa lugha ya kigeni.

Akizungumza na SUAMEDIA Makamu Rasi wa Ndaki ya Kilimo SUA Dkt. Hamisi Tindwa amesema kuwa Ndaki hiyo imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali kuhusiana na ubora wa mbegu pamoja na masuala ya udongo ili kumsaidia mkulima kufaidika na kilimo chenye tija kutokana na tafiti za kitaalamu zilizofanyika.

Dkt. Tindwa amesema kuwa wamekuwa wakijitahidi kuandaa majarida hayo na kuyaweka katika Maktaba ya Taifa ya Kilimo inayopatikana katika Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo SUA na kwa njia ya mtandao.

“Tunazo namna kadhaa za kushughulika na tafiti hizo, kwanza ni kuhakikisha matokeo ya utafiti ambayo kwa kawaida yanakuwa yamechapishwa kwa lugha ya kigeni yanatafsiriwa kwenye vijarida kwa lugha ya Kiswahili na kuwafikia watu wa kawaida nchini, na vijarida hivi tayari vipo kwenye maktaba ya Taifa ya Kilimo na bado program hii ni endelevu”, amesema Dkt. Tindwa.

Pia amesema Ndaki hii ya Kilimo inasimamia Idara ya Huduma za Ugani ambayo licha ya kufundisha Sayansi ya Ugani inashirikiana na Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza katika kuhakikisha tafiti zote zinazozalishwa zinatafsiriwa kwa namna ambayo itamfikia Mkulima wa kawaida.

Dkt. Tindwa amesema ushirikiano wa idara hizi huleta matokeo chanya katika suala la Kilimo hasa tafiti hizo zinazotafsiriwa na kumfikia mkulima wa kawaida katika kuzalisha mazao yenye tija kupitia tafiti zinazowekwa katika vijarida kwa lugha adhimu ya Kiswahili.  

Kwa kutambua umuhimu wa matokeo ya Tafiti kwa walengwa ambao ni wakulima, Ndaki hii ya Kilimo inaendelea kutoa wito kwa wakulima kufika SUA na kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo kilimo cha kisasa ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na kilimo cha mazoea.

KATIKA VIDEO


Post a Comment

0 Comments