Na: Calvin Edward Gwabara
Morogoro.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia mradi
wa VaSPHARD kwa
kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamefanya mafunzo kwa Waganga wa tiba asili na kisha kupima
dawa zao ili waweze kubadilisha mtazamo na tabia katika kuzalisha dawa ili watengeneze dawa
salama,safi na zenye viwango vya juu na kupata usajili.
Mkuu wa Mradi wa VASPHARD Dkt. Faith Mabiki akizungumza kwenye mafunzo hayo ya siku moja ya watengenzaji wa dawa za asili kutoka Mikoa mbalimbali. |
Akizungumza na SUAMEDIA Mkuu wa Mradi wa VaSPHARD Dkt. Faith Mabiki
amesema kuwa mafunzo hayo yanawakutanisha waganga wa tiba asili na
watengenezaji wa dawa zaidi ya 35 kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania
ambao wamekuja na dawa zao zaidi ya 100 ambazo baada ya majadiliano na
kujengeana uelewa wa zoezi hilo zitapimwa na kisha kupewa majibu kujua ubora wa
dawa hizo na kuwashauri namna bora za kuzalisha na kufungasha dawa zao kukidhi
viwango vya kimataifa.
“Kwahiyo sasa hivi tunajadiliana nao baada ya
kuwajengea uelewa na tunaingia nao makubaliano kisha tutakwenda maabara kufanya
vipimo viwili ambavyo vimewekwa na serikali ili waweze kutengeneza dawa
kiusalama zaidi”. Alieleza Dkt. Mabiki.
Ameongeza “Ili Serikali iweze kuzitangaza dawa hizo
lazima wapelekwe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuangaliwa vipimo kadhaa kama vile
sumu kuvu,vipomo vya wadudu wanaosababisha magonjwa au dawa kuwa chafu, vipimo
vya madini tembo na kemikali iliyo ndani
ya dawa hizo, na kwa bahati nzuri vipimo hivyo vyote SUA tunaweza kuvifanya
ndio maana Mkemia Mkuu wa Serikali ametupa kufanya baada ya kupata hela kutoka
kwa Jumuiya ya Wanataaluma wa Sayansi Afrika tunakwenda kufanya kazi hii”.
Amesema kama kweli Taifa linataka kuona Dawa
wanazotengeneza zinachangia afya ya Jamii na maisha ya wataalamu hao wa tiba asili
lazima swala la ubora wa dawa hizo lizingatiwe hapo ndipo wataweza kulifikia
soko kubwa la ndani ya Tanzania na nje kama ambavyo nchi zingine maarufu kwa
uzalishaji wa dawa hizo wamefikia mfano India na China.
Dkt. Mabiki amesema kuwa zoezi la upimaji wa dawa kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali lina gharama kubwa kama ambavyo waganga hao wamesema
lakini SUA kama taasisi ya Elimu na Utafiti wanavyo vifaa vya kisasa na bora
lakini pia wanao wanafunzi wanaofanya tafiti hizo kwenye shahada mbalimbali za
Juu ambao wanatumia dawa hizo kuzifanyia utafiti na kupata shahada zao lakini
pia waganga wenyewe wenye hizo dawa wanapimiwa dawa zao bure na kupewa ushauri
wa namna ya kufanya
Kwa upande wake Mtaalamu wa tiba asili kutoka Njombe Bw.
Flavian Nyakeji amesema amefurahi kupata nafasi hiyo ya kipekee ya kuelimishwa
na kujua namna ya kutengeneza dawa zenye ubora
“SUA imetusaidia kwa muda mrefu kuboresha utengenezaji
wa dawa zetu wanataka tufikie viwango vya juu, na sisi hili ndilo tunalolitaka
maana sisi tunaotoka Njombe tunauza Njombe tuu, likini sasa lini tutauza Dar es
Salaam, Mwanza, Kenya na lini tutauza Ulaya” amesema Nyakeji.
Nyakeji amesema ameleta dawa kumi kwenye zoezi hilo
ili aweze kujua nini kipo kwenye dawa zake hasa kwa kujua ubora wake na yupo
tayari kupata ushauri wa kitaalamu wa namna ya kuboresha dawa hizo ili ziweze
kuwa na viwango badala ya kuzalisha bila viwango hali ambayo itatunyima usajili
na kutofikia soko la nje.
Mtaalamu huyo wa Tiba asili amesema kupitia mafunzo na
uwezeshwaji huo wa kitaalamu tayari kuna mabadiliko makubwa kati uzalishaji wa
tiba asili nchini na anaamini kuwa kutafanyika mapinduzi makubwa katika soko la
tiba asili nchini na wataweza kuuza bidhaa zao nchi ya nchi kama ambavyo nchi
zingine zinauza Tanzania.
Mhadhiri wa kutoka Idara ya Sayansi ya mazao ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt. Richard Madege akiwasilisha mada yake mbele ya waganga hao wa tiba asili |
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mafunzo hayo. |
0 Comments