Na, Hadija Zahoro
Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kimesema kinajivunia kwa kutambulika na dunia nzima kwa kuwa na tafiti bora pamoja na machapisho ambayo yamenukuliwa zaidi ulimwenguni.
Hayo yamesemwa na Mteknolojia wa Kitengo cha Kompyuta kutoka Kurugenzi hiyo Bw. Kundasen Swai wakati akizungungumzia majukumu ya kitengo hicho kupitia SUAMEDIA katika kipindi cha Kapu la Leo kinachorushwa hewani na SUAFM.
Bw. Swai amesema katika kuhakikisha wanakitambulisha Chuo ulimwenguni, wanamiliki tovuti ya chuo ambayo inatumika kuweka maelezo na mambo yote yanayofanyika chuoni hapo, ikiwemo tafiti pamoja na machapisho mbalimbali ambayo yanaenda kusaidia watu wengi duniani.
“Tunahakikisha tunakitambulisha Chuo hapa ulimwenguni kwamba tunamiliki tovuti ya chuo inayotumika kuweka maelezo yote mfano tafiti, machapisho yote tunaweka huko kwenye tovuti ya chuo ambapo dunia inaweza kuingia kule na kutafuta yale machapisho na tafiti ambazo zinaenda kuisaidia dunia”, amesema Bw. Swai.
Ameeleza kuwa dunia inafanya ushindani wa vyuo vingi vilivyopo ulimwenguni ili kutambua chuo kipi kinafanya tafiti za kutosha pamoja na utoaji wa elimu mzuri hivyo Chuo cha SUA kimeshika nafasi ya pili kwa Tanzania, 51 kwa Afrika, 28 kwa Kusini mwa Jangwa la Sahara na 2033 kwa ulimwengu mzima kwa mashindano ya ujumla yaliyotolewa Mwezi Julai, Mwaka 2021.
Mteknolojia huyo ameongeza kuwa kwa takwimu hiyo iliyotolewa na dunia, Chuo cha SUA kimefanikiwa kuvipita vyuo vingi vikubwa duniani kwa kushika nafasi nzuri kwenye mashindano hayo ya jumla.
Amesisitiza kwamba ukiachana na takwimu hiyo ya mashindano ya ujumla, kwa mashindano ya tafiti bora zinazopatikana na zilizonukuliwa na watu wengi zaidi pamoja na kusaidia watu wengi, Chuo cha SUA kimeshika nafasi ya 1 kwa Tanzania kwa kuwa na tafiti bora, 32 kwa machapisho na tafiti bora Afrika na 1241 kwa ulimwengu mzima.
Aidha, amesema kupitia ubora huo wa chuo wamekuwa wakipata wanafunzi wengi kutoka nje ya nchi na duniani kwa ujumla ambao wanakuja chuoni hapo kwa ajili ya kusoma kwa sababu wanapata elimu na tafiti bora.
0 Comments