Na.Tatyana Celestine.
Watafiti na
Wadau wa kilimo wametakiwa kuimarisha ushirikiano ili kukifanya Kilimo Ikolojia
nchini kuwa na tija kwa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa
Utafiti na Uzamili kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo SUA
Prof. Ezron Karimulibo katika uzinduzi
wa Kitovu cha Kilimo Ikolojia awamu ya pili mjini Morogoro ambapo amesema Kilimo Ikolojia kinaendelea kupewa kipaumbele
nchini kwa sababu ni kilimo ambacho kinajali na kutunza mazingira na kuongeza kuwa ni kilimo kinachoweza kufaidisha
vizazi na vizazi.
‘’Katika
suala la kilimo ikolojia tunalipa kipaumbele kwa sababu ni kilimo ambacho kinajali na kutunza
mazingira lakini pia uendelevu wa vizazi
na vizazi vinaweza kunufaika na kilimo ikolojia nchini mwetu lakini zaidi ya hapo tumewaasa
watafiti na wadau wa kilimo katika
mkutano huu kuendeleza umoja kwa sababu
mazingira ya ushirikiano inabidi yaboreshwe
zaidi baada ya kipindi hiki cha UVIKO 19
kwasababu wasitazamie sana ufadhili kutoka nje ya nchi lakini tukiboresha ushirikiano wetu kwa taasisi za ndani tunaweza tukafikia malengo makuu katika
kukiendeleza kilimo hiki,’’ amesema Prof. Karimulibo .
Aidha Prof.
Karimulibo amesema kuanzia kipindi cha mwaka 2019 hadi mwaka 2020 wamewafikia wakulima
wa mikoa ya Morogoro, Arusha na Singida lengo likiwa ni kutoa elimu juu ya ulimaji wa kilimo ikolojia na jinsi wanavyoweza kupata faida kupitia
kilimo hicho.
Prof. Karimulibo
ameongeza kuwa kilimo ikolojia kinaweza kuwa mkombozi kwa wakulima kutokana na ghala za mbolea za kisasa kuwa juu
ambapo amesema zaidi ya asilimia 80 ya wakulima kote nchini wanaishi vijijini na wanategemea kilimo
kuendesha maisha yao ya kila siku.
“Tunaamini
kwamba kuja na teknolojia hii mbadala ya
kilimo ikolojia basi tunaamini tutaweza kuinua
tija na kuinua uzalishaji wa mazao yatokanayo na kilimo,” amesema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande
wake Mratibu wa Mradi wa Kitovu cha Kilimo Ikolojia Tanzania Prof. Dismas
Mwaseba amesema kuwa mradi ulianza mwaka
2019 na awamu ya kwanza imemalizika mwaka 2021 ambapo mradi umelenga
katika kuboresha maisha ya mkulima na kufanya uhifadhi wa mazingira.
”Tunategemea katika
awamu hii ya pili ambayo tunaianza mwaka huu
2022 na kukamilika 2024
tutaongeza eneo la kufanyia utafiti
kwa kuzingatia mahitaji ya wakulima, kwa ujumla wakulima wamepokea
vizuri hizi mbinu mbalimbali za kilimo ikolojia tunazowapatia na tunavyoona
serikali ikiweza kutoa msaada basi
wakulima wengi watanufaika na kilimo hiki”, amesema Prof. Mwaseba.
Akizungumzia
changamoto kubwa katika kufanya kilimo ikolojia Prof. Mwaseba amesema kuwa sera iliyopo sasa
inajikita zaidi kwenye kilimo ambacho kinahitaji matumizi makubwa ya mbolea na
viuatilifu na kuomba kuwepo kwa mabadiliko
ya kisera ambayo yatakiwezesha kilimo ikolojia nchini kuwa rahisi kwa wakulima
wote wanaotegemea kilimo kuendesha maisha yao.
Uzinduzi huo
wa kitovu cha kilimo Ikolojia awamu ya pili
umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa kilimo nchini pamoja na wakulima
ambapo mradi huo unafadhiliwa wa
MARKNIGHT FOUNDATION pamoja na DANIDA Kutoka Nchini Denmark huku ukiwa unazihusisha taasisi mbalimbali za
Serikali ikiwemo TARI, TARIRI pamoja na taasisi binafsi zinazojihushisha na
kilimo hapa nchini.
KATIKA VIDEO
0 Comments