SUAMEDIA

Rushwa imeongeza umaskini katika jamii na kuharibu mifumo ya elimu na afya

 

Gerald Lwomile

Mazumbai - Tanga

Imeelezwa kuwa kuwepo kwa rushwa nchini kwa kiasi kikubwa kumeongeza umaskini katika jamii kwa kuharibu mifumo ya kiuchumi na kupunguza uwezo wa serikali kukusanya mapato ambayo hutumika kuwahudumia wananchi


Afisa wa Takukuru wilayani Lushoto mkoani Tanga Bw. Mbangula Kumbola  akitoa ufafanuzi kwa washiriki wa mafunzo
Kauli hiyo imetolewa Februari 21, 2022 na Afisa wa Takukuru wilayani Lushoto mkoani Tanga Bw. Mbangula Kumbola wakati akitoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mazumbai juu ya watumishi wa umma na mapambano dhidi ya rushwa nchini yaliyoandaliwa na Kamati ya Kudhibiti Uadilifu (KKU) SUA

Mbangula amesema rushwa imekuwa ikiharibu mifumo ya elimu na hatimaye kuzalisha taifa lenye watu wajinga lakini pia huduma za afya zimekuwa zikizorota na hatimaye kiwango cha maradhi kwenye jamii kuongezeka

“Ikumbukwe kuwa nchi yetu ipo vitani na vita yetu ni dhidi ya maadui watatu wakubwa ambao ni Umaskini, Ujinga na Maradhi. Rushwa imekuwa ikiongeza ugumu wa kupambana na maadui hawa” amesema Mbangula

Akizungumzia namna ya kupambana na rushwa katika utumishi wa umma amesema ni muhimu kila mtumishi wa umma kutambua nafasi adhimu aliyonayo kwani watumishi wa umma ndiyo taasisi iliyokasimiwa wajibu na serikali wa kuratibu na kusimamia shughuli zote za utoaji huduma na maendeleo


Aidha amesema utiifu, kutokuwa na upendeleo, uwajibikaji, uwazi na kuepuka mgongano wa kimaslahi ni wajibu mkubwa alionao mtumishi wa umma

Awali akifungua mafunzo hayo Kaimu Msimamizi wa Misitu wa Mazumbai Bw. Chamahndi Bigingo Muriga amesema SUA kupitia KKU imeandaa mafunzo haya ili kutoa uelewa kwa watumishi kuhusu uadilifu na jinsi ya kupambana na rushwa, na namna ya mtumishi kuenenda kama mtumishi wa umma ili kuleta tija na ufanisi wakati wa kutekeleza majukumu yake.

Kaimu Msimamizi wa Misitu wa Mazumbai Bw. Chamahndi Bigingo Muriga wa pili kutoka kushoto waliokaa akiwa katika picha ya pamoja na watoa mada na wafanyakazi wa Kampasi ya Mazumbai wa pili kulia waliokaa ni Mwenyakiti wa KKU - SUA Prof. Christopher Mahonge na wa kwanza kulia waliokaa ni Katibu wa KKU - SUA Prof Yasinta Muzanila

Amesema Menejimenti ya Chuo itaendelea kuandaa mafunzo kama haya kwa watumishi wengine ili kuendelea kuboresha utendaji kazi  na kuleta mabadiliko chanya kwenye utekelezaji wa majukumu waliyonayo

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Kampasi ya Mazumbai iliyoko Bumbuli mkoani Tanga yamewashirikisha watumishi wote wa Kampasi hiyo ambayo SUA huitumia kwa tafiti mbalimbali za misitu

Post a Comment

0 Comments