Na: Winfrida Nicolaus
Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Mabinti katika Sayansi inayofanyika Februari 11 kila mwaka, Wataaluma ambao ni Wanawake katika Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo SUA wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kubadilisha vikwazo vinavyowakabili kama wanawake kuwa fursa ili kuleta maendeleo katika jamii na kuwa mfano kwa mabinti.
Picha mtandaoni |
Wito huo umetolewa na Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyama Pori na Utalii katika Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo SUA Prof. Suzan Agustino wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu siku hiyo.
Prof. Suzan amesema licha ya wanawake kulea watoto na familia kwa ujumla pia wanatakiwa kutambua kuwa hata kwenye kazi wana wajibu wao wa msingi wa kufanya tafiti mbalimbali ili kutoa elimu pamoja na ushauri kwa wadau na kuzitumia tafiti hizo kwaajili ya kutatua matatizo katika jamii na Taifa kwa ujumla
Amesema jambo la muhimu kwa wanawake ambao wamepata elimu katika fani ya Sayansi ni kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha mabinti ili kuipenda fani hiyo na kuwakumbusha kuwa kila kitu kinahitaji jitihada binafsi kwakuwa hakuna kilicho kigumu kama inavyodhaniwa kwa fani hiyo.
“Kwa jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na chuo cha SUA toka miaka ya nyuma ili kuunga mkono jitihada za Serikali na Wizara husika, idadi ya wanawake kusoma masomo ya sayansi imekua ikiongezeka ingawa changamoto bado ni nyingi, hivyo tuitumie siku hii kuendelea kuhamasisha mabinti kusoma Fani ya Sayansi na sisi tulioweza kusoma tutoke huko nje pamoja na kushiriki mijadala mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa jamii’’, amesema Prof. Suzan
Aidha amesema hamasa inatakiwa iongezeke kwa kuwa idadi ya Wanawake na Mabinti katika Fani ya Sayansi hasa kwa upande wa Uhandisi imekuwa ndogo ukilinganisha na maeneo mengine chuoni hapo.
0 Comments