SUAMEDIA

Dk Mwele afariki dunia

 


Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele katika Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Mwele Malecela amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 60.

Dk Mwele amefariki dunia  Alhamisi Februari 10, 2022 jioni mjini Geneva, Uswisi wakati akipatiwa matibabu.

Msemaji wa WHO-Tanzania amethibitisha kifo hicho.

Kabala ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele wa WHO, Dk Mwele alikuwa Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Espen), wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.

Dk Mwele ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kabla ya kuvuliwa wadhifa huo na Rais John Magufuli Desemba 17, mwaka 2016.

Kuondolewa kwake katika nafasi hiyo kulifanyika siku moja baada ya kutoa ripoti ya utafiti wa magonjwa, ndani yake ikiwamo taarifa ya virusi vya ugonjwa wa Zika katika maeneo ya Morogoro, Geita na Magharibi mwa Tanzania.

Siku moja baada ya kutoa takwimu hizo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa na Dk Mwele aliitisha mkutano na waandishi wa habari kukanusha taarifa hizo kwamba ugonjwa huo bado haujaingia nchini.

Dk Mwele aliyezaliwa Machi 26, 1962 aliwahi kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya urais mwaka 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Post a Comment

0 Comments