Na Gerald Lwomile
Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amevitaka vyuo vikuu vya
kilimo, yaani, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na Chuo Kikuu Cha Mwalimu
Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia, kuhakikisha vinabeba jukumu kubwa
katika mabadiliko ya kimuundo ya kilimo nchini.
Akifungua Kongamano la siku moja katika maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru katika Chuo Kikuu cha Mt. Augustine Jijini Mwanza leo tarehe 01 Desemba, 2021 Mhandisi Gabriel amesema ubebaji huo wa jukumu katika kilimo iwe katika maana pana ya kukuza kilimo kupitia mimea vipando, mifugo, uvuvi na mifumo ya uzalishaji wa misitu pamoja na tasnia ya kilimo inayohusiana nayo.
Amesema ni muhimu kwa Vyuo vikuu hivi kuendelea kutekeleza majukumu yake
kwa weledi kwani ni taasisi muhimu katika kuhakikisha kunakuwa na mageuzi ya
uchumi wa nchi hasa katika sekta ya kilimo.
Mhandisi Gabriel amesema Mwaka 1961 wakati Tanzania Bara inapata uhuru,
mchango wa kilimo katika mapato ya fedha za kigeni ulikuwa ni zaidi ya asilimia
75 na watanzania waliokuwa wanaendesha maisha yao kwa kutegemea kilimo walikuwa
zaidi ya asilimia 90 kati ya Watanzania milioni 9.8.
“Mchango wa sekta ya Kilimo katika Pato Ghafi la Taifa GDP ulikuwa zaidi
ya asilimia 70, wakati kilimo kilikuwa kinachangia takribani asilimia 81 ya
mapato ya mauzo ya nje. Mapato kutokana na mauzo ya mazao ya kilimo yalikuwa
Dola za Marekani Milioni 115 mwaka 1961. Kwa sasa, mchango wa kilimo katika
pato la Taifa ni wastani wa asilimia 27.2. Ukuaji huo unaonyesha kuwa kilimo
bado kinachangia kiasi kikubwa katika uchumi ingawa kiwango cha uchangiaji
kimekuwa kikishuka kutokana na kukua kwa sekta nyingine hususan madini,
viwanda, ujenzi na huduma” amesema Mhadisi Gabriel
Amesema pamoja na mafanikio haya sekta ya kilimo imeendelea kukumbwa na
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa kujikimu na usio na tija
miongoni mwa wakulima wodogo hapa nchini.
“Kwa mfano, uzalishaji wa mahindi uko chini ya tani mbili (tani 1.9) kwa
hekari moja badala ya tani 8. Uzalishaji usio na tija miongoni mwa wakulima
wadogo hutokana na sababu nyingi ikiwemo mapungufu ya huduma za ugani
yanayosababishwa na kutofikiwa kwa uwiano wa afisa mmoja kuhudumia kaya 600
(1:600) au kijiji kimoja (1:1)” amesema Mhandisi Gabriel
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amefurahishwa kuona maonesho ya
teknolojia na ubunifu katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi
yaliyofanywa na SUA katika Kongamano hilo.
Ambapo ameipongeza SUA kwa maonesho ya teknolojia mbalimbali ambazo
wamezibuni na kuahidi kuhakikisha kunakuwa na maonesho makubwa zaidi ambayo
yatasaidia wananchi na wakulima mbalimbali katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Awali akimkaribisha
Mkuu huyo wa Mkoa ili kufungua Kongamano hilo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema kongamano hilo ni muhimu ili
kutoa uelewa wa mambo mbalimbali kwa wakulima ikiwa ni pamoja na namna ya
kuzikabili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo
Prof.Christopher Kasanga Mkuu wa Idara ya Mikrobiolojia SUA akiwaeleza wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ngaza namna wanavyotumia mashine za kisasa kutambua vimelea vya magonjwa kwa njia ya vinasaba
Prof. Chibunda
amesema katika miaka 60 ya Uhuru SUA imefanikiwa kutoa wataalamu mbalimbali wa
kilimo ambao wamesaidia kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inakua kwa kufanya
tafiti na kutoa huduma mbalimbali za ugani hususani kwa wakulima waliko
vijijini
Aidha ameongeza
kuwa SUA imeendelea kuzalishaji miche ya matunda ikiwemo kwa njia ya chupa,
kutoa chanjo za wanyama na uthibiti wa visumbufu vya mazao ya kilimo na wanyama
Naye Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia Prof Lesakit Mellau
akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi amesema Serikali imekuwa ikiunga mkono
juhudi za kilimo nchini ikiwa ni pamoja na kuendelezwa kwa ujenzi katika vyuo
vinavyotoa elimu ya kilimo nchini
Kongamano hilo la kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru lililofanyika leo
Desemba 01, 2021 na kubeba kauli mbiu isemayo ‘Mchango wa Sekta ya Kilimo katika
Maendeleo ya Tanzania: Mafanikio na Changamoto Miaka 60 Baada ya Uhuru’.
limeshirikisha chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Mwalimu
Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia, na mwenyeji Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Agustino cha Tanzania (SAUT)
0 Comments