Na. Winfrida Nicolaus
Wachumi na Wadau wa Kilimo kutoka mikoa mbalimbali nchini wametakiwa kuhakikisha wanafanya tafiti ambazo zitakuwa chachu kwa wakulima sanjari na kuhakikisha maarifa waliyokuwa nayo yanawafikia wakulima pamoja na kuishirikisha Serikali katika maazimio mbalimbali ambayo wanakubaliana.
Hayo yamesemwa Decemba 01, 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Raisi, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohamed kwenye Mkutano wa 13 wa Jumuiya ya Wataalam wa Uchumi Kilimo unaofanyika kwa siku tatu Mkoani Morogoro
Dkt. Salum Mohamed amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinaendelea na kuwa kilimo cha kisasa na cha kibiashara, kitakacho mnufaisha mkulima mdogo mdogo lakini vilevile kinakuwa ni kilimo ambacho kitasaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi ya Tanzania
Amesisitiza kuwa jambo la muhimu ni kumpatia soko mkulima na baadae mkulima lazima azalishe mazao kwa kiwango kinachokubalika katika soko lakini pia ni jukumu lake kuongeza uzalishaji,
“Kubwa zaidi ni kuhakikisha kwamba ili kuleta kilimo cha kibiashara basi mkulima badala ya kuwa ni mkulima anayetumia jembe la mkono na mtoto mgongoni abadilike na kutumia dhana za kisasa, mbegu bora lakini vilevile awe na utaratibu wa kutumia maji kwaajili ya umwagiliaji na kuzalisha zaidi ”, amesema Dkt. Mohamed
kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wachumi Kilimo Tanzania Bw. Felix Adam Nandonde amesema katika mkutano huo yatawasilishwa mawasilisho ya kitaalam 24 kutoka kwa wachumi kilimo na wadau mbalimbali ambao wanafanya tafiti au kuendeleza kilimo na wakulima wake pia.
Amesema wao kama wataalam kutokana na mawasilisho hayo watahakikisha mkulima wa kitanzania anaondoka katika dhana ya kutegemea mvua za msimu ama Kudra za mwenyezi Mungu pamoja na kuondoka katika kilimo cha kienyeji cha kutumia jembe la mkono kwa kumpatia mkulima maarifa ya kutosha.
“Sisi kama wataalam wa kilimo na uchumi kilimo tunaamini moja ya njia kubwa ama suluhu mojawapo ni kuhakikisha tumewajengea uwezo wakulima wetu kwa kuimarisha vyama vya msingi vya awali kwa kuvijengea uwezo kuwa na watendaji mahiri na menejimenti yenye uelewa tunaamini vyama hivi vinaweza kuwa chachu ya kuweza kubadilisha kilimo cha Tanzania” amesema Bw. Nandonde
Aidha amesema ili kujenga na kuimarisha kilimo nchini jambo la lazima ni kuhakikisha wakulima wanaaandaliwa kwa kupatiwa maarifa sahihi na wanakuwa na uelewa wa kutosha.
0 Comments