- Ezekiel Kamwaga
- Mchambuzi
Desemba 9 mwaka 1961 - mambo makubwa mawili yalifanyika kama sehemu ya maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika; Mosi ilikuwa ni kushusha chini bendera ya mkoloni na kupandisha ya taifa huru na wakati huohuo kupandisha Mwenge wa Uhuru kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Tukio la kupandisha bendera lilifanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, uwanja uliojengwa mahsusi kwa ajili ya sherehe za uhuru na umuhimu wake ulikuwa kuonesha kuondoka kwa mkoloni na kwamba kuanzia wakati huo - Watanganyika watakuwa huru kufanya mambo yao wenyewe kwa mustakabali wao.
Kushushwa kwa bendera ile kulikuwa ni tukio kubwa kwa waliolishuhudia. Kuna wazee wa zamani wanazungumza kuhusu vilio vya furaha vilivyosikika wakati wa tukio hilo lililofanyika saa sita usiku.
Kule Kilimanjaro, tukio hilo halikujulikana maana yake sana hadi pale Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipozungumza maneno yafuatayo kuhusu tukio hilo; ""Tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu; ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini; upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau".
Miaka 60 baada ya Uhuru wa Tanganyika - sasa ikifahamika zaidi kwa jina la Tanzania kutokana na Muungano wake na Zanzibar mwaka 1964, ni wakati wa kutafakari na kuona kama taifa hili lipo pahali ambapo wale waliopigania Uhuru walitaka iwe wakati huu.
Kuhusu Uhuru
Ingawa Nyerere alikuwa Waziri Mkuu - kwa maana ya Mkuu wa Serikali, na Malkia wa Uingereza akiendelea kuwa Mkuu wa Dola walau katika mwaka wa kwanza wa Uhuru, Tanzania ilikuwa huru kujiamulia mambo yake.
Katika miaka ya kwanza ya Uhuru, Tanzania ilijipambanua kama taifa linaloamini katika Umajumui wa Afrika - Nyerere akielezwa kuwa tayari kusubiri Tanzania isiwe huru ili Jomo Kenyatta aachiwe kutoka jela Kenya - kuja kuwa Rais wa Shirikisho la Afrika Mashariki na kushiriki katika harakati za kumkomboa mtu mweusi barani Afrika na kwingine duniani.
Katika elimu, Tanzania ilianza kufanya jitihada za makusudi za kusomesha watu wake, kuanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na vyuo vingine vya kistadi kiasi kwamba kufikia mwishoni mwa miaka ya 1970, ilikuwa ikitajwa kuwa mojawapo ya nchi zilizofuta ujinga kwa kiasi kikubwa duniani huku UDSM ikitajwa kama mojawapo ya vitovu vya fikra za kimapinduzi barani Afrika.
Tanzania pia ilianzisha viwanda vingi vilivyotumia malighafi kutoka kwa wakulima na wazalishaji wengine wa Tanzania na ingawa vipato havikuwa vikubwa - taifa hilo lilikuwa na ajira za kutosha kwa vijana wake waliomaliza kwa viwango mbalimbali vya elimu.
Katika diplomasia ya kimataifa, Tanzania pia ilikuwa mojawapo ya mataifa mashuhuri na yenye sauti - ikitoa viongozi wa kaliba ya Dk. Salim Ahmed Salim, kwenda kuongoza katika vyombo mbalimbali vya kimataifa.
Hata hivyo, wakosoaji wa Tanzania wanaeleza pia kwamba kasoro kubwa kwenye taifa huru hilo ilikuwa ni kuamua kuminya uhuru wa watu wake - kuanzia ule wa maoni na haki za kiraia.
Miaka michache baada ya Uhuru, Nyerere alitangaza Tanzania kuwa nchi inayofuata mfumo wa chama kimoja -TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwa hatua hiyo, wote walioonekana kupingana na uamuzi huo walichukuliwa kama maadui.
Ni kutofautiana huko kwa mawazo ndiko kulisababisha - kwa upande wa Zanzibar, baadhi ya wanasiasa maarufu kama Abdulla Kassim Hang ana wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Kwa sababu ya kukosekana kwa uwajibikaji kwa wahusika wa matukio mabaya ya watu kufungwa, kupotezwa na kushughulikiwa kisiasa kwa sababu ya tofauti za kimtazamo, matukio kama hayo bado yanajirudia miaka 60 baada ya Uhuru.
Tanzania imefika ilikotaka?
Kizazi cha kwanza cha watawala wa Tanzania kilifanikiwa kufanya jambo moja kubwa; kuunganisha watu kutoka makabila, dini, mila na tamaduni tofauti na kutengeneza nchi ya watu wanaojiita Watanzania.
Na kwa kuangalia kuhusu vigezo kama ujenzi wa barabara, ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa huduma na bidhaa muhimu kwa maisha ya watu, Tanzania imepiga hatua kubwa kulinganisha na hali ilivyokuwa miaka 60 iliyopita.
Karibu mikoa yote ya Tanzania sasa inaweza kufikika ndani ya saa 24 au 48 kwa usafiri wa mabasi na idadi ya vifo vya watoto wanaofariki dunia chini ya miaka mitano inapungua kila kukicha.
Hata hivyo, bado inatatizwa na mambo ambayo pengine waliopigania Uhuru wa Tanzania hawataamini kama yanatokea sasa. Kwa mfano, kama ambavyo inaonekana sasa, bado kuna matatizo yanayosababisha nchi isiwe na uhakika wa umeme na maji.
Hili ni jambo ambalo maelezo yake ni magumu kwa sababu Tanzania ina kila kitu cha kuifanya isiwe na shida ya maji wala umeme miaka 60 baada ya Uhuru. Kuna upepo, maji, gesi na nishati mbadala za kutosha kuifanya isiwe na matatizo ya nishati.
Kuhusu Uhuru na Haki
Kama kuna changamoto kubwa zaidi kwa watawala wa sasa Tanzania ni changamoto kubwa kwenye masuala ya haki. Huko nyuma, taifa hilo liliwasha mwenge kupeleka mwanga kwenye giza na matumaini kule kule uonevu.
Kwenye miaka ya karibuni, kumetokea matukio ambayo yametia doa kubwa katika juhudi za kujenga utaifa na utu miongoni mwa Watanzania.
Matukio ya kuvuruga uchaguzi, kubana haki za kiraia za wananchi, kupotezwa kwa wat una wanasiasa wenye muono tofauti kufunguliwa kesi kwenye mahakama za nchi yameanza kuwa ya kawaida.
Huko nyuma - miaka michache kabla ya Uhuru, matukio ya namna hii yalikuwa yakihusishwa na serikali ya kikoloni na wananchi walipigana kutaka Uhuru wao.
Watanzania, wakati ule, walipigana ili wapate haki ya kuchagua viongozi wao waliowataka, kuzungumza matatizo yao kwa uwazi, kutofungwa bila makosa au utu wao kutwezwa kwa namna yoyote ile.
Ikrari, katika mapambano dhidi ya Uhuru, watu wengi hawakupigania Uhuru kwa sababu ya kutaka mambo ambayo yanaonekana kwa macho au kushikika mkononi kama vile reli, maji na barabara.
Wananchi walichoka kunyanyaswa. Walichoka kumwona mgeni akitawala mahali pasipo kwake. Walichoka kufanywa raia wa daraja la pili. Walitaka mawazo yao kwenye mustakabali wa nchi yasikike.
Ndiyo sababu, wakataka mmoja katika wao ndiyo apatikane kuwaongoza ili kutimiza ndoto zao. Mmoja atakayewasikiliza, kuwaheshimu na kuwathamini.
Pasi na shaka, jambo la wananchi limebaki kuwa hilo hata sasa. Swali pekee la kuuliza ni kama - miaka 60 baada ya Uhuru, Tanzania ilipo ndipo hasa waasisi walitaka iwe au la?
CHANZO BBC SWAHILI
0 Comments