Jaribio la ulinzi wa anga katika eneo la Natanz katikati mwa Iran lilisababisha mlipuko uliosikika takriban kilomita ishirini kutoka eneo la nyuklia la Chahid Ahmadi-Rochan.
Msemaji wa jeshi amedai kuwa mlipuko huo ulitokana na majaribio ya mfumo wa makombora ya kuzuia ndege katika eneo hilo. Jaribio hili linakuja baada ya kuzuiwa kwa mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na mataifa makubwa huko Vienna. Mazungumzo yalisitishwa kwa wikendi hii na yataanza tena katikati ya wiki ijayo.
Katika wiki za hivi karibuni, Israel imehakikisha kwamba itachukua hatua kwa kila njia kusitisha shughuli za nyuklia za Tehran. Ikiwa ni pamoja na kwa nguvu, alibaini Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Yaïr Lapid mwezi Oktoba.
Na hivi majuzi, tarehe 2 Disemba, Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett alitoa wito kwa Marekani "kumaliza mara moja" mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran katika mahojiano ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.
"Iran inafanya 'usaliti wa nyuklia' kuwa mbinu ya mazungumzo na jibu la hili lazima liwe kumalizika mara moja kwa mazungumzo na kuchukuliwa hatua madhubuti za madola makubwa" dhidi ya Tehran, Bennett alisema wakati wa mazungumzo hayo.
Mnamo mwezi Julai 2020, kitendo cha hujuma kilisababisha uharibifu mkubwa kwa moja ya majengo katika eneo la Natanz, ambapo vifaa vipya vya mtambo wa kisasa vilikusanywa. Wakati huo, Iran iliishutumu Israeli kwa kuhusika na hatua hiyo. Kwa mujibu wa Tehran, Israel pia ilifanya hujuma dhidi ya mtambo wa uzalishaji wa centrifuge ulioharibika karibu na Tehran.
Iran imeongeza kwa kasi shughuli zake za kurutubisha madini ya uranium katika eneo la Natanz lakini pia katika eneo la Fordoo, lililo chini ya mlima takriban kilomita mia moja kutoka Tehran. Hii inafanya hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya eneo hili kuwa ngumu sana.
Shughuli hizi zimeshutumiwa vikali na nchi za Magharibi na Israel, ambazo zinaituhumu Iran kwa kutaka kutengeneza silaha ya atomiki au kuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
0 Comments