NA: Calista Nyimbo
Wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamekumbushwa kufuata sheria, taratibu na miongozo inayotolewa ya kamati hiyo ili kuboresha ufanisi wa kazi na kutimiza malengo ya Chuo.
“Mimi nina matumaini makubwa sisi sote tunaoshiriki mafunzo
haya tutakuwa wasikivu na tutajipa muda ili kuelewa na kukubali kukumbushwa
majukumu na umuhimu wa shughuli za ukaguzi katika kusimamia majukumu ya Chuo” ,amesema
Prof. Chibunda.
Prof. Chibunda amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya
Utekelezaji wa Mpango kazi wa Kamati ya Ukaguzi ya mwaka wa fedha 2021/2022 na
ni sehemu ya kutekeleza Hati Idhini ya Kamati kuwa yatolewe mafunzo mafupi kwa
wanakamati wa kamati ya ukaguzi.
“Kama wengi wetu tunavyofahamu Kamati hii ndio jicho la Baraza
katika usimamizi kuhakikisha kwamba utendaji wetu unazingatia kanuni, taratibu,
sera, mifumo na miongozo mbalimbali ya kiserikali na ile ambayo inatolewa na
Baraza letu la Chuo”, amesema Prof. Chibunda.
Pia ameelezea dhumuni la mafunzo hayo kuwa ni kuwaongezea
uelewa kamati ya ukaguzi na kuwakumbusha majukumu yao na umuhimu wa kamati ya
ukaguzi katika kushauri Baraza la Chuo kwenye utekelezaji wa majukumu yao
hususani katika usimamizi wa chuo.
Aidha ameongezea kuwa mafunzo hayo yalihusisha pia Menejimenti
ya Chuo kutokana na Kamati ya Ukaguzi kufanya kazi karibu na Menejimenti hiyo
hivyo mafunzo hayo yatawasaidia wote kuelewa pamoja masuala muhimu ya Usimamizi wa Rasilimali za
Chuo na kujiandaa na viatarishi mbalimbali vinavyokikabili Chuo hicho.
Naye mtoa mada katika mafunzo hayo ambaye ni Muasisi wa Taasisi ya Ukaguzi wa ndani (TIA) Godfrey
Kilenga ameshukuru kwa mualiko alioupata kutoka SUA kutoa mafunzo hayo na
kwamba ana Imani yataleta mabadiliko makubwa Chuoni hapo.
Amesema kuwa miongozo mingi ya shughuli za ukaguzi inatoka
serikalini hivyo ni vizuri wajumbe hao
kufanyia kazi yatakayofundishwa ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na
kutimiza malengo waliyojiwekea.
0 Comments