Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Mathayo Maselle amekipongeza na kukishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kuzalisha wahitimu ambao wanajiajiri na kusaidia kuanzisha miradi ambayo inachangia kutoa maarifa na kuzalisha ajira kwa vijana wengine nchini.
Mkuu huyo wa wilaya amesema
kuwa kupitia fursa hiyo vijana wanakwenda kujiajiri na kutengeneza uchumi huku
halmashauri ikienda kupata mapato.
“Vijana waitumie hii
fursa ni fursa muhimu sana ambayo haichoshi kwa kuwa unaweza ukaifanya huku
ukiwa unafanya shughuli yako nyingine, kama hawajawaambia vizuri kazi yako ni
ndogo ukishakuwa na mzinga wako umejua mahali pa kuuweke kauweke pale kaendelee
na shughuli zako za shamba ukisubiri kwenda kuvuna asali”, amesema Maselle.
Aidha amewataka vijana waliopata fursa hiyo na wananchi wote waliopata taarifa kuzitumia
vizuri fursa zilizopo za misitu pamoja na kutunza maeneo ili kuweza kufaidika
na fursa hiyo ya uvunaji wa nyuki.
Aidha Maselle ameongeza
kuwa akiwa kama mmoja kati ya wahitimu wa SUA anaunga mkono juhudi hizo zilizoletwa
na ACLA HONEY huku akihakikisha matokeo
ya kile ambacho kimekusudiwa yanaonekana .
Akielezea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo muwakilishi wa
Mkurugenzi wa Kampuni ya ACLA HONEY, Giovanni Nguvu amesema kampuni hiyo
ambayo imetokana na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia
taasisi ya SUGECO ina mashamba kwenye mikoa saba ya Tanzania yenye mizinga
7,000 na kampuni yao huzalisha asali tani zaidi ya 25,000 kwa mwaka na soko
kubwa la asali yao ni nje ya nchi.
Alisema kutokana na uzoefu wa kampuni hiyo na uaminifu umekuwa
ukitekeleza miradi mbalimbali nchini na sasa wamepata ufadhili wa kutekeleza
mradi huu ambao utahusisha wilaya mbili za Malinyi na Ulanga na utawafikia
vijana 1500 moja kwa moja wenye umri kati ya miaka 14 hadi 24 na kati yao 500
wakitoka wilaya ya Ulanga na 1,000 wakitoka Wilaya ya Malinyi.
“Mradi huu una malengo ya kukuza kipato cha kaya na kuongeza lishe
kupitia ufugaji wa nyuki wa kisasa ambapo pamoja na wanufaika kuunganishwa
kwenye vikundi na kupatiwa mafunzo lakini pia watapewa mizinga ya kisasa ya
ufugaji wa nyuki, vifaa vya kulina asali na mazao mengine ya nyuki na
kuhakikishiwa soko la mazao yote ya nyuki yatakayozalishwa”, alieleza Nguvu.
Nguvu ameongeza kuwa maf unzo
hayo pia yatakwenda mbali zaidi kwa kuwafundisha mbinu bora za kuongeza thamani
mazao yatokanayo na nyuki kama vile kutengeneza Mishumaa, ving’arisha viatu,
ving’arisha Midomo, Mvinyo pamoja na bidhaa zingine nyingi.
Amesema Mradi huo kwa sasa upo kwenye hatua za majaribio kwa
kipindi cha miezi saba kutoka mwezi wa nane hadi wa tatu mwakani na
pindi Mfadhili atakaporidhishwa na matokeo ya utekelezaji ya mradi basi awamu
kuu ya miaka minne ya Mradi itaanza Mwezi Mei 2022 hadi mwezi Aprili 2026.
0 Comments