Na Farida Mkongwe
Serikali
wilayani Morogoro imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa uamuzi
wa kuanzisha Shule ya udereva wa mitambo ya kilimo, magari na pikipiki ambao
utapunguza matumizi ya nguvu kazi katika uzalishaji na hivyo kusaidia taifa
kufikia malengo ya uzalishaji chakula.
Pongezi hizo
zimetolewa na Mkuu wa wilaya ya Morogoro Bw. Abert Msando wakati wa ufunguzi wa
shule hiyo uliofanyika Novemba 19, 2021 kwenye viwanja vya Kampasi ya Edward
Moringe mjini Morogoro.
Bw. Msando
amesema pamoja na shule hiyo ya udereva kulenga wanafunzi wa SUA lakini pia
itakuwa ni fursa ya kuwafundisha vijana wengine kupata ujuzi wa namna ya
kuendesha mitambo mbalimbali ya kilimo na hivyo kuwa njia mojawapo ya kuwafikia
wakulima wengi nchini.
Amesema SUA
imekuwa Chuo Kikuu cha mfano nchini katika kubuni na kuibua Miradi na Programu
mbalimbali zinazolenga kuwajengea vijana uwezo na kuwawezesha kujipatia ajira
hususani katika sekta ya kilimo na kilimo biashara
“Chuo hiki
ni cha kwanza kutoa mafunzo ya mitambo ya kilimo na udereva katika nchi yetu
yanayoendeshwa na Chuo kikuu, vijana watakaojifunza katika shule hii watapata
fursa ya kukutana na wataalam waliobobea katika fani mbalimbali zikiwemo za
udongo, mimea, uhandisi kilimo na umwagiliaji na fani nyingine za kilimo cha kisasa......",
alisema Bw. Msando.
Awali
akimkaribisha mgeni rasmi Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda
amesema SUA baada ya kupokea matrekta 10 kutoka kwa Hayati Rais John Magufuli
kilijitathmini na kuona sababu za msingi za kuanzisha shule hiyo kwa ajili ya wanafunzi wa SUA
ambao hasa mitaala yao inawataka kujifunza udereva na ufundi wa mitambo hiyo.
“Shule hii
itasaidia sana wanafunzi wetu kupata mafunzo, cheti na leseni ya utumiaji wa
mitambo ya kilimo (Daraja G) na kuwasaidia kupata ajira au kujiajiri pale
wanapohitimu masomo yao na pia itasaidia kuifikia jamii yenye uhitaji wa
mafunzo na ujuzi wa kuendesha mitambo ya zana za kilimo hususani vijana”,
alisema Prof. Chibunda.
Mafunzo ya
Shule hiyo yatakayotolewa kwa awamu nne kwa mwaka yatakuwa ya muda wa wiki tano
hadi nane kutegemeana na aina ya kozi na awamu ya kwanza itaanza mwezi Januari
na Februari mwakani.
0 Comments