Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua “Ajira Portal Mobile App” itakayotumiwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuendesha mchakato wa ajira Serikalini ambao utaondoa vitendo vya rushwa na upendeleo kwa waombaji wa ajira.
Akizindua portal hiyo leo jijini Dodoma, Mhe.
Mchengerwa amesema portal hiyo itasaidia kuwapata watumishi wenye sifa stahiki
na wazalendo watakaolitumikia taifa kwa weledi, uadilifu na wataolifikisha
taifa kwenye uchumi wa kati wa juu.
Mhe. Mchengerwa amesema, mfumo huo wa maombi ya
kazi kupitia simu ya kiganjani umelenga kuwapunguzia adha mbalimbali walizokuwa
wakikutana nazo waombaji wa fursa za ajira ikiwemo upatikanaji wa taarifa
zinazohusu ajira serikalini na mchakato wake.
“Mfumo huu ukitumika vizuri, ninaamini waombaji
wa ajira wataweza kufanya maombi ya ajira popote walipo mijini na vijijini,
kwani mfumo unamuarifu muombaji uwepo wa nafasi.
Mhe. Mchengerwa amewahamasisha waombaji wa ajira
serikalini kuanza kutumia mfumo huo ambao utapunguza changamoto nyingi
walizokuwa wakikabiliana nazo kabla ya uwepo wa mfumo huo.
Akimkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzungumza na
Watendaji na wadau wa ajira, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameipongeza Sekretarieti
ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Mchengerwa ya
kuwataka kuanzisha mfumo utakaorahisisha mchakato wa ajira kwa waombaji wa
ajira serikalini.
“Nakumbuka katika kikao chako cha kwanza
uliporipoti ofisini, ulikuwa na maono ya kufanya mchakato wa ajira kuwa wa
kidijitali na kuelekeza mfumo huo uundwe ili kurahisisha mchakato wa ajira
Serikalini, na hatimaye leo unazindua rasmi mfumo huo,” Mhe. Ndejembi
ameongeza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amesema maono ya Mhe.
Mchengerwa yanaenda sambamba na utekelezaji wa azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu
Hassan ambaye amekuwa akisisitiza mara kwa mara kufanya maboresho ya utoaji wa
huduma katika taasisi za umma kupitia TEHAMA.
Akitoa neno la utangulizi, Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kukamilika
kwa mfumo huo wa Ajira App ni hatua kubwa iliyofikiwa na ofisi katika
kurahisisha mchakato wa ajira serikalini kwa kutumia TEHAMA.
Ili kuhakikisha Sekretarieti ya Ajira inautumia
mfumo huo ipasavyo, Dkt. Ndumbaro ameiomba Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma iliyozinduliwa hivi karibuni kushirikiana na watendaji wa
Sekretarieti ya Ajira katika usimamizi wa mfumo huo ili uwe na manufaa kwa
umma.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu
ya ofisi yake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw.
Exavier Daudi amesema huduma hiyo ya Mobile App itaongeza wigo wa
upashanaji habari za ajira na kuokoa fedha ambazo waombaji walikuwa wakizitumia
kulipia huduma za mtandao kwa wafanyabiashara wa huduma hizo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi wakati wa uzinduzi wa Ajira Portal Mobile App leo jijini Dodoma. |
0 Comments