Na. Veronica
Mwafisi-Pangani
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
amewataka Watumishi wa Umma kutotanguliza mbele masilahi binafsi katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo na badala yake wafikirie njia sahihi ya kutekeleza
miradi hiyo ili kuleta tija kwa taifa.
|
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo kwa Viongozi na Watumishi wa Wilaya ya Muheza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhe. Halima Bulembo na kulia kwake ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Rasilimaliwatu na Utawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Sebastian Masanja. |
Mhe. Ndejembi ameyasema
hayo Wilayani Muheza wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya hiyo
iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa
miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo.
Mhe. Ndejembi amesema,
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo hivi karibuni ametoa kiasi
cha shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, vituo vya afya na
ununuzi wa vifaa mbalimbali hivyo, watumishi wanaohusika na utekelezaji wa
miradi hiyo wasimamie kikamilifu na kwa weledi mkubwa badala ya kufikiria
watapata nini kutoka kwenye fedha hizo.
“Mhe. Rais Samia Suluhu
Hassan amekuwa akipeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwenye
halmashauri, hivyo tulinde rasilimali hizo na kuwa wabunifu katika kuweka njia
sahihi za utekelezaji wa miradi hiyo.” Mhe. Ndejembi amesema na kuongeza kuwa
mtumishi akiwa mbunifu na kutekeleza majukumu yake kwa weledi anaisaidia Serikali
kufikia malengo ya maendeleo kwa taifa.
Aidha, Mhe. Ndejembi
amesema kukosekana kwa maadili kwa baadhi ya watu kumesababisha baadhi ya
watumishi wanaoajiriwa kutaka maisha mazuri na kumiliki vitu vya gharama hali
inayosababisha kuingia kwenye rushwa kutokana na kutamani vitu wasivyokuwa na
uwezo navyo.
“Leo hii, kuna watu
wakiajiriwa, badala ya kutekeleza kazi kwa weledi, wanataka kesho wamiliki gari
na nyumba nzuri, hapo ndipo rushwa na udokozi vinaanza kwasababu ya kutamani
vitu ambavyo wanajua kwa muda wao bado,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Katika kukabiliana na
tatizo hilo, Mhe. Ndejembi amewasistiza waajiri kuwapeleka Chuo cha Utumishi wa
Umma Watumishi wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza Serikalini kabla ya kuanza
kutekeleza majukumu yao ili wapate elimu itakayowawezesha kutekeleza majukumu
yao kwa weledi na kuiishi miiko ya Utumishi wa Umma.
Mhe. Ndejembi ameendelea
na ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na
kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Jiji la Tanga ambapo leo alikuwa
Wilayani Muheza.
|
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Wilaya ya Muheza jijini Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhe. Halima Bulembo na kulia kwake ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Rasilimaliwatu na Utawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Sebastian Masanja.
|
|
Mtumishi wa Wilaya ya Muheza kutoka Idara ya Mifugo, Bibi Ruth Mwilongo, akiwasilisha hoja za kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo. |
|
Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Wilaya ya Muheza jijini Tanga wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo. |
0 Comments