Na farida Mkongwe
Serikali wilayani Morogoro imeanza utaratibu wa kuandaa na kutekeleza Mkakati shirikishi wa kutunza na kulinda vyanzo vya maji na mazingira kama njia mojawapo ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji.
![]() |
PICHA KUTOKA MAKTABA |
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bw. Abert Msando wakati akizungumzia changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji iliyopo kwa sasa katika ufunguzi wa shule ya udereva wa mitambo ya kilimo, magari na pikipiki uliofanyika SUA mjini Morogoro.
Bw. Msando amesema uamuzi huo umefikiwa kutokana na kipindi kigumu kilichopo kwa sasa kwani iwapo mvua hazitanyesha ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia leo Novemba 19, 2021 basi maji yatapungua kwenye bwawa la Mindu kwa zaidi ya asilimia 50 hivyo hakutakuwa na maji kutoka chanzo hicho.
“Ni lazima tuseme kwa uwazi na ukweli ili kila mtu atambue kulikuwa na mito mitano inayoingiza maji katika bwawa la Mindu lakini kwa sasa umebaki mto mmoja tu ile mingine yote maji yake yamekauka”, alisema Bw. Msando
Amesema sababu kubwa za changamoto ya upatikanaji wa maji ni kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye vyanzo vya maji zikiwemo shughuli za kilimo, ufugaji na uchimbaji madini ambazo sasa zimesabisha mgao wa maji kuwa mkubwa.
Amesema katika kukabiliana na hali hiyo sasa suala la kulinda na kutunza vyanzo vya maji na mazingira sio la hiari tena bali ni lazima na kwamba wadau wa mazingira wakiwemo SUA, TAFORI, NEMC, Wakala wa Huduma za Misitu TFS na Halmashauri ya wilaya pamoja na wadau wengine wanapaswa kufanya jitihada za kuokoa mazingira.
![]() |
PICHA KUTOKA MAKTABA |
0 Comments