SUAMEDIA

Mkuu wa Chuo SUA Jaji Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba afurahishwa na mafanikio katika kipindi cha miaka mitano ya Uongozi wake

 26/10/2021                        MOROGORO                    ZIARA

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba ametoa pongezi kwa Makamu Mkuu wa Chuo, Baraza la Chuo na kwa Wafanyakazi kwa ujumla kwa kazi kubwa iliyofanyika katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano chuoni hapo.



Jaji Warioba ametoa pongezi hizo Octoba 26, 2021 katika hafla fupi iliyohusisha Viongozi na Wafanyakazi wa SUA ikiwa ni hitimisho la ziara yake ya siku mbili Chuoni hapo akiwa ameambatana na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Mhe. Jaji Mstaafu Mohamed Othman Chande, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Bi. Dorothy Mwanyika, Mkewe Mama Warioba na viongozi wengine wa chuo hicho. 

Jaji Warioba amesema katika ziara zake alizofanya kwa miaka mitano chuoni hapo kuna utofauti mkubwa na ukarabati umefanyika kwa kiwango kikubwa katika Kampasi hizo mbili za Edward Moringe na Solomon Mahlangu hususani katika miundombinu ya barabara pamoja na majengo.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda akitoa ripoti na taarifa ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Jaji Warioba, amesema Chuo kimepata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha asilimia 96.4 ya mapato yaliyokusudiwa, kupanda kwa ubora wa Chuo, utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo kwa upande wa utafiti Chuo kilishika nafasi ya 51 barani Afrika na ya kwanza kitaifa.

Akieleza changamoto zilizopo Chuoni hapo, Prof. Chibunda amesema Chuo kimekuwa na upungufu mkubwa wa Wafanyakazi wanataaluma, ufinyu wa bajeti hususan bajeti ya maendeleo na mchakato wa miundombinu ya barabara za chuo na kuongeza kuwa wamelenga kuboresha mazingira ya ufundishaji, kuweka mifumo ya kusimamia fedha zinazopatikana na kuongeza umakini na uadilifu katika matumizi.

Aidha, ameongeza kuwa serikali kwa kushirikiana na wizara ya elimu imetenga sh. billion 74.2 ambazo wamepanga kuzitumia kujenga majengo mapya na kuboresha miundo mbinu ya chuo na hivyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SUA na Jaji mstaafu Mohammed Othman Chande amesema Baraza lake kwa kipindi cha miaka mitano limetekeleza mambo mbalimbali ikiwemo kusimamia uanzishwaji wa Kampasi ya Mizengo Pinda na kusimamia matumizi ya mpango mkakati wa chuo na kumpongeza Jaji Warioba  kwa Miongozo, Ushauri na Maelekezo kwa baraza hilo


KATIKA VIDEO

Post a Comment

0 Comments