Na.Vedasto George
Waandishi wa habari mkoani Morogoro wamesisitizwa kuwa
wazalendo na kufanya kazi kwa kufuata misingi,taratibu ya taaluma ya habari
ikiwemo kutanguliza masilahi ya Taifa.
Msisitizo huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bw.
Bakari Msulwa katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ambayo
ufanyika kila ifikapo tarehe 3 mei na kusema kuwa kitu pekee ambacho kinaweza
kumtambulisha muandishi wa habari katika jamii na Taifa ni jinsi anavyofanya
kazi kwa kufuata misingi ya taaluma hiyo ubunifu na kutanguliza maslahi ya Taifa.
Msulwa ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita itaendelea
kuheshimu na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na vyombo vya habari nchini
huku akibainisha kuwa Serikali pia itaendelea kuweka
mazingira mazuri ya ufanyaji kazi kwa wanahabari pamoja na upatikanaji wa habari
zenye mlengo wa kujenga Taifa.
Aidha Msulwa amekitaka Chama cha Wahandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro kuanzisha Miradi mbalimbali ya Maendeleo ambayo itawawezesha
waandishi wa habari mkoani humo kuweza kujipatia kipato nje na kazi yao wa
uandishi wa habari.
Kwa upande wao baadhi ya waandishi wa habari akiwemo
Simon Mogela na Dastani Ibraimu wameiomba Serikali kuziangalia upya Sharia
zinazoongoza Vyombo vya Habari ili kuweza kutoa fursa kwa wanahabari
kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kote
duniani uadhimishwa kila ifikapo Mei 3 kila mwaka ambapo Maadhimisho ya mwaka
huu yalibebwa na kaulimbiu isemayo "HABARI KWA MANUFAA YA
UMMA"


0 Comments