Na: Calvin Gwabara
Watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
wameshauriwa kuhakikisha wanaweka fedha kwa ajili ya kusambaza matokeo ya
utafiti kwa walengwa na kuchangia katika kutengeneza sera au kuziboresha
wanapoandika maandiko ya miradi yao kwa wafadhili.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Utafiti na machapisho
katika Kurugenzi ya Shahada za Uzamili,Utafiti,Uhaulishaji wa Teknolojia na
ushauri wa kitaalamu SUA Prof. Japhet Kashaigili wakati akifunga hafla fupi ya
kufunga mradi wa kuwezesha matokeo ya tafiti ili kuzaa sera iliyofanyika kwenye
Kampasi ya Solomon Mahlangu ya Sayansi na Elimu.
Prof. Kashaigili amesema kumekuwa na tafiti nyingi nzuri
ambazo zinafanywa na watafiti wa SUA lakini bado mchango wake haujaonekana sana
katika kusaidia utungaji wa sera na uboreshaji wa sera zilizopo na matokeo yake
zinatumika kwenye kuwapatia watafiti shahada na kupanda madaraja.
‘’ Ukiangalia hata swala la usambazaji wa matokeo ya tafiti zetu mara nyingi tunaweka hela kidogo sana na muda mwingine hatuweki kabisa kwenye baadhi ya miradi ninayoifahamu lakini hili linafanyika bila kujua kuwa uchakataji wa matokeo ya utafiti husika ili kupata sera ni sehemu ya usambazaji wa matokeo kwa walengwa na kutokuweka bajeti maana yake huna kitu cha kusambaza’’ Alisema Prof. Kashaigili.
Ameongeza kuwa kwa sasa kuna ulazima kwa kila mtafiti
kujua mbinu muhimu za namna ya kuandika matokeo hayo ili yawafikie walengwa wa
utafiti kwa kuandika kwa ufupi na kutumia lugha inayoleweka kirahisi ili
kufikisha ujumbe
Katika hatua nyingine Prof. Kashaigili amepongeza uongozi
wa mradi huo kwa kuamua kuwakutanisha wadau mbalimbali wa Chuoni hapo kuwaeleza
malengo ya mradi na matokeo yake
Awali akifungua hafla hiyo Mkuu wa idara ya Mipango, Sera
na Utawala ya Ndaki ya Sayansi ya jamii na Humanitia Prof. Fatihia Massawe
amesema ili kuhakikisha kile watafiti wanafanya kinazaa sera wasitegemee
utafiti mmoja pekee maana hauwezi kumshawishi mtunga sera kutengeneza sera bali
zifanyike tefiti nyingi kwenye mitazamo tofauti kama vile Uchumi, Kijamii na
hata kiafya.
‘’Ili tuweze kupeleka andiko letu la kusaidia kuzaa sera lazima tuhakikishe limeshiba kwa maana limegusa kila eneo kwa mapana yake kwani kuna taarifa nyingine zinazobeba andiko lako la sera la sivyo tutaendelea kubaki hapa tulipo sasa tukitaka kila utafiti na kila mradi uzae sera’’ Alisisitiza Prof. Fatihia.
Akizungumzia malengo ya mradi huo wa miezi sita Mkuu wa
Mradi Dkt. Faith Mabiki amesema malengo ya hafla hiyo ilikuwa ni kuwaktanisha
wadau wote chuoni hapo kujua nini walikuwa wanafanya kwani kumekuwa na tafiti
nyingi zinafanyika chuoni hapo lakini mtafiti mmoja hajui mtafiti mwingine
anafanya nini na amepata matokeo gani.
Amesema kuwa malengo ya mradi huo ni kutaka kuona kama
watafiti wanaweza kuchangia kwenye kuzalisha sera za nchi au kuboresha sera
zilizopo ili kupata sera nzuri kutokana na utafiti,kujenga uelewa miongoni mwa
watafiti na watunga sera kuona umuhimu kutumia matokeo ya utafiti
kuzalisha sera na kujenga uwezo kwa watafiti katika kuandika matokeo yao
kwa lugha nyepesi
0 Comments