SUAMEDIA

Wakuu wa SADC walaani uasi wa Magaidi nchini Msumbiji

 


Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC wameahidi kwamba, watatoa jibu mwafaka dhidi ya hujuma na mashambulio ya hivi karibuni ya magaidi wenye mfunganao na Daesh huko nchini Msumbiji.



Viongozi wa mataifa sita wa jumuiya hiyo waliokutana Maputo mji mkuu wa Msumbiji ikiwa yamepita majuma mawili tangu kutokea mashambulio mabaya zaidi ya kigaidi huko Msumbiji wamesema kuwa, hujuma kama hizo za kigaidi hazipaswi kubakia bila majibu ya nchi za eneo.

Aidha taarifa ya pamoja ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC imesisitiza kusaidia juhudi za kudumisha amani na usalama nchini Msumbiji. Hata hivyo taarifa hiyo haikueleza ni msaada wa aina gani utakaotolewa na mataifa hayo kwa ajili ya kupambana na vitendo vya ukosefu wa usalama huko nchini Msumbiji.

Viongozi hao waliokutana ambao ni sehemu ya mataifa 16 ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC wamesema wanataraji kukutana kwenye mkutano mwingine wa kilele utakaojadili mzozo huo Aprili 29, ili kuangazia namna watakavyokubaliana kulishughulikia tatizo hilo kikanda.

Magaidi hao wanaofungamana na kundi la kigaidi la Daesh walifanya uvamizi na kuuteka mji wa Palma mkoani Cabo Delgado huko Msumbiji mnamo Machi 24 ambapo makumi ya watu waliuliwa na maelfu kulazimika kuukimbia mji huo.

Mji wa Palma uko karibu maili sita kutoka mradi mkubwa wa gesi asilia katika eneo la Afungi katika Bahari ya Hindi karibu na mpaka wa Msumbuji na Tanzania.

Jeshi la Msumbiji linasema limefanikiwa kuukomboa kikamilifu mji huo wa Palma na kwamba, watu wameshaanza kurejea katika makazi yao ili kuona madhara na wizi uliofanywa na magaidi hao.

 

Post a Comment

0 Comments