Na Gerald Lwomile
Tukuyu
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema
kinajivunia kwa kiasi kikubwa kuwa mshiriki katika miradi mbalimbali ya
maendeleo ikiwemo ile inayonyanyua na kuboresha maisha ya watu moja kwa moja
kwa kuinua kipato na kuongeza afya kwa watanzania
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo akizungumza na wadau hawapo pichani, kulia ni Mratibu wa Mradi Prof. Dismas Mwaseba
Hayo yamesemwa Aprili 14, 2021 na Mkurugenzi wa
Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam
Prof. Esron Karimuribo ambaye amemwakilisha Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala wakati akifungua warsha ya siku moja ya kisera
katika kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa chakula, Mradi ujulikanao kwa jina la
‘Innove Africa’
Prof. Karimuribo amesema ushiriki wa SUA katika Mradi huu unasaidia kufanikisha malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkakati namba mbili wa kidunia katika kuhakikisha inaondoa baa la njaa hadi ifikapo mwaka 2030
“Mradi huu ulijikita katika kuhakikisha unapanua
kilimo hiki cha nyasi hizi za Brachiaria kama njia mbadala ya kuweza kupata
malisho bora ambayo yataongeza uzalishaji wa maziwa yenye ubora zaidi na kwa
hivyo kupitia uzalishaji huo basi mfugaji anapouza maziwa anaongeza kipato
lakini pia yakitumiwa na wanajamii yanaongeza lishe”, amesema Prof. Karimuribo
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo ambao ulikuwa
unaangalia namna bora ya kukuza nyasi aina ya Brachiaria ili kuongeza
uzalishaji wa maziwa nchini, Mradi unaofanyika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya
Mratibu wa Mradi huo Prof. Dismas Mwaseba amesema wao kama watafiti wameona
mbegu aina ya Brachiaria inastawi zaidi katika Ukanda huo wa Nyanda za Juu Kusini
na kwa kiasi kikubwa unaweza kuwa msaada kwa wafugaji katika eneo hilo
Aidha amesema kuwa kupitia Jukwaa la Ubunifu na Jukwaa
la Wafugaji wa ng’ombe kama litatumiwa vizuri lina uwezo wa kueneza kilimo hiki
chenye manufaa makubwa kwa wafugaji na hasa katika kuhakikisha kilimo kinaendelea
kikiwemo kilimo cha nyasi
Nao wakulima mbalimbali wanaoshiriki katika Mradi huu
wamesema kwa sasa wanaona manufaa ya mradi huo na hasa baada ya ongezeko la
uzalishaji wa maziwa na upatikanaji wa nyasi hizo tofauti na awali
Nyasi za Brachiaria katika mwonekano wake halisi (Picha zote na Gerald Lwomile)
Mfugaji Bibi Mehne Mwasumbi na Stanley Salingo wamesema
tangu walipopanda nyasi hizi wamekuwa na raha wakati wote kwani kwa upande wa
Mwasumbi hata kama mumewe hayupo hutoka tu nje ya nyumba yao na kukata nyasi na
kulisha ng’ombe lakini pia anaona tofauti ya maziwa ambapo kwa sasa ubora wake
umeongezeka kwa kiasi kikubwa
0 Comments