SUAMEDIA

Zaidi ya Shilingi Bilioni 73 zimepelekwa Mkoa wa Tanga kutekeleza Miradi ya Elimu

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Mkoa wa Tanga umepaokea jumla ya Sh bilioni 73 na milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu. 



Makamu wa Rais amesema hayo Wilayani Korogwe Mkoani Tanga wakati akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Chuo cha VETA Korogwe ambapo amesema ahadi ya Serikali ni kuendelea kuwasomesha watoto wa kitanzania kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne bila malipo pamoja na kujenga shule za sekondari, Vyuo vya Ufundi na Vyuo Vikuu vya kutosha.

 Amesema ameridhishwa na miradi ya Serikali inayotokelezwa katika mkoa wa Tanga ikiwepo ujenzi wa VETA mpya katika halmashauri ya Korogwe na kutaka ikamilike kwa wakati ili iweze kutoa elimu na ujuzi kwa vijana katika Mkoa wa Tanga. 

"Tanga inakua kwa viwanda vinavyojengwa na vitahitaji wataalamu, hivyo VETA Korogwe ikikamilika ichukue vijana ili tupate wataalamu watakaofanya kazi kwenye viwanda,"amesisitiza Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu

 Nae Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Chuo cha Ufundi VETA Korogwe ni moja kati ya Vyuo vya vya ufundi 25 vinavyojengwa katika halmashauri mbalimbali nchini kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Ujuzi na Kazi ambapo Serikali ilitenga Sh bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo na kwamba ujenzi wake unasimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA.

Amesema sambamba na kujenga VETA hizo bado zipo VETA nne ambazo zinajengwa kupitia Halmashauri ambazo ni Ruangwa, Kasulu Kongwa na Nyasa na kufanya VETA zinazojengwa kufikia 29 na kwamba zitakuwa zimekamilika kufikia Juni 2021 na kuanza kudahili. 

 "Baada ya VETA hizi kukamilika, Mwezi Julai 2021 tunatarajia kudahili wanafunzi ambapo tutaongeza udahili wa wanafunzi elfu 24 mia sita na hamsini,"alisema Waziri Ndalichako

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa amesema wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia Chuo cha Ufundi VETA Korogwe kwa kuwa kitataoa fursa kwa vijana wa Halmashauri ya Korogwe na Tanga kwa ujumla kupata ujuzi na Maarifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema ujenzi wa VETA Korogwe umefikia asilimia 65 ambapo mpaka kukamilika utagharimu Sh bilioni 1 na milioni 600. 

Aliongeza kuwa mradi utakapokamilika mwezi Mei 2021 Chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili jumla ya wanafunzi 840 kati yao 240 ni wa kozi za muda mrefu na 600 wa kozi za muda mfupi kati ya miezi mitatu na sita.

Post a Comment

0 Comments