Na
Gerald Lwomile
Katavi
Wafanyakazi
na wanafunzi katika Kampasi zote za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
wameshauriwa kutokuwa na woga katika utoaji taarifa za ukiukwaji wa uadilifu.
Hata hivyo, taarifa hizo ziwe za kweli si majungu.
Wito
huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kuthibiti Uadilifu (KKU) SUA, Prof.
Christopher Mahonge wakati akizungumza na wafanyakazi katika Kampasi ya Mizengo
Pinda iliyoko mkoani Katavi. Amesema utoaji wa taarifa za kweli utasaidia
kuyashughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa uadilifu ipaswayo ili kuhakikisha
sehemu ya kazi inakuwa mahali pazuri na salama kwa kila mfanyakazi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuthibiti Uadilifu (KKU) SUA, Prof. Christopher Mahonge akifafanua jambo kwenye mkutano na wafanyakazi hawako pichani (Picha na Gerald Lwomile)
Naye Naibu Rasi wa Ndaki kwa upande wa Taaluma wa
Kampasi ya Mizengo Pinda, Prof. Anna Sikira, amesema katika kuhakikisha maadili
yanafuatwa katika sehemu ya kazi ni muhimu kwa watumishi kuhakikisha wanafuata
miongozo mbalimbali ya kazi.
Prof.
Sikira amesema miongozo hiyo inajumuisha matumizi ya lugha sahihi katika eneo
la kazi, kufika na kutoka kazini kwa wakati, kuingia darasani kwa wakati,
kutimiza wajibu, na kuwa na mahusiano mazuri ya kikazi katika eneo la kazi.
Hayo ni miongoni mwa mambo muhimu katika kutimiza uadilifu.
Naibu Rasi wa Ndaki kwa upande wa Taaluma wa Kampasi ya Mizengo Pinda, Prof. Anna Sikira akisisitiza juu ya uadilifu kwa wafanyakazi
Katika
hatua nyingine mjumbe wa KKU Dkt. Abdul Katakweba, akizungumza na wanafunzi
katika Kampasi ya Mizengo Pinda, amewataka wanafunzi hao kuzingatia maadili yakiwemo
ya uvaaji mavazi yenye staha kwa wanafunzi wote wa kike na wa kiume. Pia Dkt.
Katakweba amewashauri wanafunzi hao kuzingatia kikamilifu masomo yao kwa sababu
hicho ndicho kitu kilichowaleta chuoni.
Mwenyekiti wa KKU Prof. Mahonge wa pili kulia akiwa na Naibu Rasi wa Ndaki kwa upande wa Taaluma wa Kampasi ya Mizengo Pinda, Prof. Anna Sikira wa kwanza kushoto na wajumbe wa KKU
0 Comments