Na Gerald Lwomile
Katavi
Wahadhiri katika vyuo mbalimbali, wakiwemo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wameaswa kuepuka kupokea zawadi kutoka kwa wanafunzi ambazo haziko katika mfumo rasmi kwa kuwa zinaweza kuwaingiza katika mtego wa kupokea rushwa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati
ya Kuthibiti Uadilifu (KKU) SUA, Prof. Christopher Mahonge, wakati akijibu
swali kutoka kwa Mhadhiri Elisha Luta wa Kampasi ya Mizengo Pinda ya Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo iliyoko Mkoa wa Katavi aliyetaka kujua kama mwanafunzi
ataamua kumpa zawadi mwalimu kwa kufundisha vizuri inaweza kutafsiriwa kuwa ni rushwa?
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuthibiti Uadilifu (KKU) SUA, Prof. Christopher Mahonge akifafanua jambo kwa wafanyakazi wa Kampasi ya Mizengo Pinda (hawapo pichani) Picha zote na Gerald Lwomile
Prof. Mahonge akizungumza na
wafanyakazi hao, wakiwemo wahadhiri katika Kampasi ya Mizengo Pinda ya SUA, amesema
kuna uwezekano wanafunzi kumshawishi mwalimu kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kutoa
zawadi, jambo linaloweza kumfanya mwalimu kutoa upendeleo au kutowajibika
ipaswavyo katika utekelezaji wa majukumu yake kama njia ya kulipa fadhila.
Akizungumza namna ya utoaji taarifa kwa
Kamati ya Kuthibiti Uadilifu Prof. Mahonge amesema wafanyakazi na wanafunzi wanaweza
kutumia njia mbalimbali kama vile kutuma taarifa kupitia kwa mwakilishi wa wafanyakazi/wanafunzi,
au kupeleka taarifa moja kwa moja kwa wajumbe wa KKU kwa kupiga simu au kutumia
baruapepe au kwa kutumia masanduku ya maoni. Hii itasaidia endapo itatokea njia
moja ya upokeaji wa taarifa ina changamoto ya mgongano wa kimasilahi.
Prof. Christopher Mahonge amesema ili
kuepuka vikwazo katika utoaji wa taarifa wanafunzi na wafanyakazi wote wamepewa
fursa ya kutoa taarifa kwa kwa njia ya simu, baruapepe na masanduku ya maoni. Hata
hivyo, ameonya kuwa taarifa zinazotolewa zisiwe za majungu kwa sababu
zinasababisha rasilimali fedha, watu, muda na mahali kutumiwa kwa njia ya hasara.
Naibu Makamu Mkuu wa Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. Anna Sikira aliyekaa kulia akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi na wajumbe wa KKU, waliokaa katikati ni Mwenyekiti wa KKU Prof. Mahonge na kushoto ni Katibu wa KKU Prof. Muzanila
Naye Katibu wa Kamati ya Kudhibiti Uadilifu
SUA Prof. Yasinta Muzanila amesema katika kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji
na uadilifu katika maeneo ya kazi ni muhimu wafanyakazi waliofanya kazi kwa bidii
wakatambuliwa kwa mfano kwa kupewa tuzo, kama vile barua au cheti,
zitakazotambua mchango wao katika maeneo yao ya kazi.
Amesema ili kuwepo na
maendeleo nchini ni muhimu kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo
nchini kwa kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Rushwa katika maeneo ya
kazi.
Katibu wa Kamati ya Kudhibiti Uadilifu SUA Prof. Yasinta Muzanila akifafanua jambo kwa washiriki wa mafunzo ya uadilifu
Prof. Muzanila amesema kuwa kama hakuna
amani, utulivu na uwajibikaji wananchi hawatapata huduma katika eneo husika na
kuwa uwazi na uadilifu utasaidia jamii kutumia rasimali nyingi zilizopo kwa uhakika
0 Comments