Na :Samirah Yusuph
Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Maswa (MAUWASA) mkoani Simiyu imekamilisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chujio la kutibu na kusafirisha maji katika bwawa la New Sola wilayani humo ulio asisiwa 1970 na Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere na kusanifiwa upya 2008 kisha kuanza kukarabatiwa 2016.Mradi huo ulioghalimu kiasi cha Sh3.5 bilioni umekarabatiwa kwa muda wa miaka 4 ukiwa unauwezo wa kuzalisha mita za ujazo wa maji 10,365 kwa siku na kuhudumia wananchi zaidi ya 111, 400 pamoja na mifugo 100,000.
Ambapo katika ukarabati wake umejumuisha ujenzi wa majengo mawili (jengo la kuchanganyia madawa, jengo la uendeshaji wa mitambo) pamoja na chujio kwa ajili ya kutibu maji na kuyasafirisha katika tenki tayari kwa matumizi ya viumbe hai.
Akizungumzia ukarabati huo kaimu meneja wa MAUWASA Nandi Mathias amesema kuwa ujenzi wa chujio jipya pamoja na ukarabati wa mitambo ulilenga kuboresha huduma ya upatikanajia wa maji pamoja kuboresha mitambo ili kuendana na ubora wa chujio.
Ambalo lina uwezo wa kuchuja mita za ujazo wa maji 10,365 kwa sasa linazalisha mita za ujazo 5,600 huku mahitaji yakiwa ni mita za ujazo 7,000 na mkakati wa kuongeza uzalishaji ukiwa ni kujenga tenki jingine la maji ambalo litakuwa na ukubwa ambao unaendana na uzalishaji halisi wa maji katika chujio hilo.
"Changamoto inayokwamisha kufikia malengo ya uzalishaji wa maji ni upatikanaji wa umeme, umekuwa ukikatika mara kwa mara jambo ambalo linapelekea uzalishaji wa maji kubaki kuwa mdogo...
Pamoja na kuwa umefungwa mtambo kwa ajili ya kudhibiti matumizi makubwa ya umeme (power factor correction) ambao utapunguza matumizi ya umeme kutoka Sh45 milioni kwa mwezi hadi kufikia Sh25 milioni matarajio ikiwa ni kufikia Sh15 milioni kwa mwezi".
Mradi huo wa maji una eneo lenye ukubwa wa ekari 937 ikijumuisha bwawa ambalo ni chanzo kikuu cha maji pamoja na eneo la hifadhi ya bwawa hilo lililopandwa miche ya miti 22,000 eneo ambalo wananchi wa wanaopakana na chanzo hicho iliwalazimu kuhama na kulipwa fidia ya Sh176 milioni ili kupisha mradi huo
Ambapo baadhi ya wananchi waliopisha mradi huo wamesema kuwa kwa sasa wameamua kukitunza chanzo hicho cha maji baada ya kuwa wamelipwa fedha zao hapo awali waligoma kufanya hivyo wakisubiri malipo fidia.
"Hapo awali hatukuelewa umuhimu wa bwawa hili kwa sasa tumeamua kuachana na shughuli za kilimo pembeni ya bwawa na sisi wenyewe tumeamua kuwa walinzi wa eneo hilo ili kulinda mifugo kufanya malisho pembeni mwa bwawa na hata kuzuia wananchi kulima," anaeleza Mbuki John mkazi aliyelipwa fidia kupisha eneo la chanzo cha maji.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa MAUWASA Paulina Ntagaye ameeleza mkakati wa kulinda chanzo hicho cha maji kuwa ni pamoja na wananchi kushiriki kuwafichua wale wote wanaohujumu miradi ya maji.
Aidha amewataka wananchi kuwa waaminifu katika kufanya malipo ya maji ili kuwezesha mradi wa maji kujiendesha na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mwisho.
0 Comments