SUAMEDIA

Utafiti uliyofanywa na Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA umebainisha kuwa usawa wa kijinsia unaimarika

 

Na: Calvin Edward Gwabara.

Utafiti uliyofanywa na Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA umebainisha kuwa usawa wa kijinsia unaimarika na kuzingatiwa sana kwenye vijiji vinavyoshiriki miradi ya uhifadhi shirikishi wa Misitu kupitia Shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania -TFCG.

Hayo yamebainika na Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii Prof. Suzan Augustino  wakati wa uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti mbele ya wadau wa Misitu mjini Morogoro na kusema kuwa jitihada kubwa zimefanywa na TFCG na Mtandao wa Jamii wa Usimaizi wa Misitu Tanzania MJUMITA kwa kuhakikisha jamii yote inashirikishwa na inanufaika na rasilimali zitokanazo na Misitu hiyo.


Rasi wa Ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii  SUA, Prof. Suzan Augustino akiwasilisha matokeo ya utafiti huo wa masuala ya kijinsia kwa wadau wa uhifadhi shirikishi wa misitu  nchini.

“ Kuna mabadiliko chanya kwenye vijiji ambavyo TFCG na MJUMITA wanatekeleza miradi yao hasa wa Mkaa Endelevu ikilinganishwa na vijiji vilivyo nje ya Mradi ingawa wanaume wanaongoza kwenye kazi zinazohitaji nguvu” alibainisha Prof. Suzan.

Prof. Suzan amesema kuwa kwenye Mradi wa Mkaa Endelevu wanawake wanakuja juu katika kushiriki kwenye biashara hiyo ijapokuwa wao wanatumia fedha kulipa watu kufanya kazi zao kama vile kukata magogo, kuyakusanya na kupanga tanuri la mkaa kazi ambazo zinaonekana kuhitaji nguvu zaidi.

Ameendelea kusema kuwa baadhi ya vijiji vina ushiriki mdogo wa wanawake na hiyo kwa mujibu wa utafiti wao wamesema inasababishwa mila na  destuli zao kwamba kazi za maporini hufanywa na wanaume tu na sio wanawake ingawa mitazamo hiyo imeanza kufutika taratibu baada ya jitihada za TFCG na MJUMITA za kutoa elimu.

Kwa upande wake Prof. John Jackoniah Mtafiti kutoka Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia - SUA amesema pamoja na mafanikio hayo ya kuongeza uwiano wa kijinsia kwenye jitihada za usimamizi shirikishi wa Misitu na matumizi ya mapato ya rasilimali hizo lakini wanaume ndio wameonekana kunufaika zaidi.


Prof. John Jackoniah ambaye ni mmoja wa watafiti kutoka Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA  akiwasilisha sehemu ya utafiti huo wa mbele wa wadau hao wa misitu mjini Morogoro.


Akieleza lengo la Utafiti huo Mkurugenzi msaidizi wa TFCG Bwana Emmanuel Lyimo amesema masuala ya kijinsia yametengenezewa mkakati mahususi wa kuhakikisha yanazingatiwa kikamilifu kwa kuwa ni swala mtambuka kwenye maendeleo.


Amesema baada ya kutekeleza mradi kwa muda sasa wameona wafanye utafiti huo ili kuona namna maswala hayo yanavyozingatiwa na kutafuta njia za kuboresha zaidi kama kuna vitu vinakosekana kupitia mapendekezo ya watafiti hao kutoka SUA.


Mkurugenzi msaidizi wa Shirika la TFCG bwana Emmanuel Lyimo akieleza malengo ya utafiti huo uliofanywa na watafiti kutoka SUA kabla ya kuanza rasmi kusikiliza matokeo hayo ya utafiti.

Utafiti huo umefanyika katika vijiji 10 wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro ambapo umeonyesha kuwa wanaume ndio wanakuwa na sauti zaidi kwenye maamuzi na hata kwenye kugawana rasilimali za misitu kwenye maeneo hayo.


Baadhi ya wadau kutoka TFCG,MJUMITA, Wizara ya Maliasili na Utalii,Waandishi wa habari na maafisa Misitu kutoka halmashauri za wilaya wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo hayo.



Post a Comment

0 Comments