Na Farida Mkongwe, Dar es Salaam
Vyuo Vikuu nchini vimetakiwa kuanzisha programu za masomo zinazoendana na rasilimali zilizopo pamoja na kuboresha maisha ya watanzania kwa kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo, afya, madini, mafuta na gesi.
Mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Dkt. Leornad Akwilapo aliyesimama kushoto akibadilishana mawazo na Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA katikati mara baada ya kutembelea banda la SUA
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu kutoka Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leornad Akwilapo wakati akifungua Maonesho
ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Dkt. Akwilapo amesema iwapo vyuo vikuu nchini
vitakuwa na programu za masomo zinazoendana na mahitaji ya watanzania basi hata
suala la kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu halitakuwepo na
badala yake wagonjwa watatoka nje ya nchi kuja kupata matibabu hapa nchini kama
ambavyo inafanyika kwa sasa ambapo baadhi ya vituo vinapokea wagonjwa kutoka
nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Wadau mbalimbali wakisikiliza hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi hayupo pichani, katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam
"Tusingependa kuwa tunapeleka wagonjwa wetu
nje kutibiwa bali nchi za nje ndio zilete wagonjwa wake hapa nchini,
tulishaanza hivyo tuzidi kujiimarisha zaidi ili na sisi tuwe kama India ambapo
watu wanapeleka wagonjwa wao kila siku", alisema Dkt. Akwilapo.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amezitaka
taasisi zote za vyuo vikuu nchini kutafuta namna ya kupanua udahili wa vyuo
hivyo ili kuendana na kasi la ongezeko la udahili lililopo kuanzia ngazi ya
shule za msingi ambalo linatokana na uamuzi wa serikali wa kutoa elimu bure kwa
shule za msingi
"Ongezeko hili likifikia hatua ya vyuo
vikuu ni wazi vyuo vyenu vitaathirika, wito wangu vyuo vyote mjipange kuanzia
sasa kuhakikisha muda utakapofika kusiwe na taharuki bali kuwe na nafasi za
kutosha wanafunzi kuweza kujifunza", alisisitiza Dkt. Akwilapo.
Akizungumzia upande wa tafiti, Dkt. Akwilapo
ametoa wito kwa vyuo vikuu na taasisi zote za utafiti nchini kujielekeza katika
kutoa tafiti zenye lengo la kujenga msingi wa uchumi wa viwanda hususani tafiti
za teknolojia na bidhaa za viwandani.
Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa
Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu na Wakuu wa Vyuo Vikuu Vishiriki vya
Tanzania Prof. Raphael Chibunda ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo SUA ameiomba Tume ya Vyuo Vikuu nchini TCU kuyapanua
maonesho hayo ili vyuo vipate nafasi ya kuonesha shughuli nyingine zinazofanywa
na vyuo hivyo zikiwemo tafiti na ushauri.
0 Comments