SUAMEDIA

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimewataka watafiti kutoa maoni yatakayojenga Sera itakayosaidia nchi.




Na. Ayoubu Mwigune

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimewataka watafiti kutoa maoni yatakayojenga Sera itakayosaidia nchi kwani tafiti nyingi zimeandikwa lakini zimeishia kubakia maktaba na kutofanyiwa kazi ipasavyo kutokana na lugha ngumu iliyotumiwa kuandikia tafiti hizo.

Akifungua Warsha iliyoandaliwa na Mradi wa CREPEE SUA na kufanyika katika  Ukumbi wa ICE, SUA  kwa niaba ya Makamu wa Mkuu wa Chuo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) Prof. Maulid Mwatawala amesema umefika wakati watafiti kuhakikisha wanaisaidia nchi kwa kutoa mawazo yao na kutengeneza sera nzuri na zinazoeleweka kwa wananchi.



Prof. Mwatawala amesema kuwa lengo warsha hiyo ni kuwafundisha watafiti jinsi ya kutumia takwimu zao na kuziweka katika lugha nyepesi ambayo watunga Sera wanaweza kutumia kufanya maamuzi katika kufanya maendeleo.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Kemia na Fizikia Ndaki ya Solomon Mahlangu Dkt. Faith Philemon Mabiki ambaye ni mtafiti mkuu wa mradi wa CREPEE unaofadhiliwa na AFIDEP shirika linaloshughulika na namna ya kuwezesha Sera ameeleza kuwa warsha hiyo imejumuisha Wakurugenzi wanaoshughulika na tafiti kutoka Vyuo visivyopungua 8 kutoka Tanzania, Wanafunzi, Wahadhiri na Watafiti wanaofanya tafiti kutoka SUA na Vyuo vingine.

Aidha ameeleza kuwa lengo kuu ya Warsha hiyo ni kujenga uwezo wa namna ya kuzisanifu tafiti na kuziweka  pamoja zikaeleweka kwa walaji na Serikali ili ziweze kuchangia Sera na maendeleo ya nchi ya Tanzania.

Akitoa shukurani   Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha cha Sayansi na Teknolojia cha Afrika Nelson Mandela Prof. Anthony Mshandete  amesema kuwa warsha hiyo imewajengea uwezo na uelewa wa jinsi ya kuchukua  matokeo ya tafiti yaliyofanywa na kuyaweka kwenye lugha ambayo inaeleweka kwa watunga sera na wanachi ambao ni watumiaji wa tafiti.












Post a Comment

0 Comments