Na; Mwandishi Wetu – Moshi, Mkoani Kilimanjaro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameagiza uongozi wa Kiwanda cha kuzalisha bidhaa za ngozi cha Karanga kutafuta masoko ndani na nje ya nchi Pamoja na kuandaa mikakati ya mauzo ambayo itahakikisha ukuaji wa soko na uuzwaji wa bidhaa za ngozi zitakazo zalishwa kiwandani hapo.
Maagizo hayo ameyatoa mara baada ya kuwasili kiwandani hapo alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kilichopo Moshi, Mkoani Kilimanjaro, Waziri Mhagama alieleza kuwa wakati hatua ya pili ya ujenzi wa mradi (Lot 2) inaendelea ni vyema idara ya masoko ikaandaa mikakati ya mauzo ambayo italenga katika kukuza soko la bidhaa zitakazokuwa zinazalishwa katika kiwanda hicho.
“Ni matarajio yangu kuwa watendaji kwa kushirikiana na idara ya masoko mna mikakati madhubuti ambayo itawafanya muweze kuwa wabunifu katika kuzalisha bidhaa zenye ubora kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa ili bidhaa hizo ziuzike katika soko la ndani na nje ya nchi, msisubiri uzalishaji uanze ndio muanze kutafuta masoko hayo” alieleza Mhagama
Waziri Mhagama alieleza kuwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) uliamua kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambalo alilitoa mwaka 2016 kwamba uwekezaji kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ieleke kwenye miradi yenye tija, PSSSF na Jeshi la Magereza nchini wanatakiwa kuongeza kasi na nguvu ya ujenzi katika hatua hii ya pili ya ujenzi wa mradi huo ili kiwanda hicho kikamilike kwa wakati.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha ujenzi wa kiwanda hiki cha kuchakata bidhaa za ngozi unakamilika kwa wakati na ni matumaini yangu kiwanda hiki kitakuwa mfano mzuri wa kuigwa Afrika Mashariki, ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na barani zima la afrika kutokana na bidhaa bora zitakazokuwa zikizalishwa kiwandani hapa,” Alieleza Waziri Mhagama
“Kama kiongozi wa mradi huu nitahakikisha malengo yote yaliyoadhimiwa katika mradi huu yanatimia na kiwanda kinaanza kufanya kazi ya uzalishaji mapema,”
Aidha Waziri Mhagama alifafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imejipanga kufanya majadiliano ya karibu na Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Idara ya Uwekezaji, Taasisi na Vyuo vya Mafunzo kuona namna bora itakayowahakikishia wanakuza soko la bidhaa zitakazokuwa zinazalishwa katika kiwanda hicho ili mapato yatakayopatikana yaweze kukuza uchumi wa nchi zaidi.
“Nchi yetu ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa ngozi, hivyo kukamilika kwa kiwanda hiki itakuwa ni ishara nzuri ya kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi zitakazo kuwa zinazalishwa kiwandani hapo, vilevile bidhaa hizo zitaingizia nchi yetu fedha za kigeni kupitia masoko ya nje” alisema Mhagama
Sambamba na hayo alitoa maagizo kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha anasimamia mikataba yote ya mradi huo ili kila jambo lolote lililopangwa kutekelezwa katika mradi huo likamilike kwa wakati.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe alisema kuwa kiwanda hicho ni muhimu na kitasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa taifa pamoja na kutoa fursa ya ajira kwa wingi.
Naye, Mkurungenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Hosea Kashimba alisema kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri PSSSF kama wabia wa mradi huo watayafanyia kazi na mahitaji yote yanayohitajika katika mradi huo yatawasilishwa kwa wakati ili mkandarasi aweze kukamilisha ujenzi huo.
Aliongeza kuwa, hadi sasa tayari mitambo ya kuchakata ngozi imeshawasilishwa kiwandani hapo na karibuni wataalam kutoa nchini Italia watawasili kwa ajili ya kuisimika mitambo hiyo pamoja na kutoa mafunzo elekezi kwa wataalum wa ndani katika kiwanda hicho.
Pia, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Mhandisi Masud Omar amesema kuwa tayari wameshaanza kufungua maduka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoani Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza. Katika Jiji la Dodoma wanatarajia kutafuta eneo ili mchakato wa ufunguzi uanze.
Alieleza pia matarajio yao ni pamoja na kutafuta mawakala wenye uzoefu wa kuuza na kusambaza bidhaa za ngozi ndani na nje ya nchi.
0 Comments