SUAMEDIA

Sekta ya Mifugo inaweza kuchangia zaidi ya asilimia 7.9 ya pato la Taifa

Na Calvin Gwabara
Dodoma

Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bwana Amos Kulwa Zephania amesema Sekta ya mifugo inaweza kuchangia zaidi ya asilimia 7.9 ya pato la taifa  endapo Serikali na wadau wengine watawekeza zaidi katika kuondoa changamoto zinazoikabili sekta hiyo

Amos Kulwa Zephania ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi  wa habari za mifugo nchini kutoka vyombo mbalimbali vya habari iliyoandaliwa na Shirika la ANSAF ili kujadili changamoto na fursa zilizopo kwenye sekta hiyo hapa nchini.

Bwana Zephania amesema pamoja na Tanzania kuwa nchi ya pili kwa wingi wa mifugo barani Afrika baada ya kugawanywa kwa nchi ya Sudan lakini bado mifugo inachangia asilimia ndogo kwenye pato la taifa huku ikikua kwa asilimia 4.9 tu.



Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi bwana Amos Kulwa Zephania (Katikati) Akitoa neno kwa wanahabari(hawapo pichani) wakati akifungua warsha ya siku mbili kwa waandishi nguli wa habari za mifugo nchini kutoka vyombo mbalimbali vya habari.


“Kwa makadirio yetu mwaka 2020 tutakuwa na Ng’ombe milioni 32.2, Mbuzi milioni 20, Kuku wa asili na wa kisasa watakuwa milioni 79.1 na nguruwe milioni 2 hivyo lazima tujiulize rasilimali  hizi zote zinatusaidia nini na kama uzalishaji wetu wa maziwa kwa mwaka ni lita bilioni 2.7 wakati matumizi yetu ni asilimia 47 kwa mwaka” Alisema Zephania.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa watu hawatumii bidhaa za ndani zinazotoka kwenye mifugo hivyo waandishi wa habari wasaidie kutoa elimu juu ya faida zinazotokana na bidhaa zetu za ndani huku akibainisha kuwa Wizara inafanya mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo ili kuhakikisha inatoa mchango unaostahili katika pato la taifa lakini kwa wafugaji na washiriki wa nyororo  wa thamani wa mifugo.

Amesema kupitia oparesheni Zagambo ya kukamata bidhaa feki za mifugo kutoka nje na zilizoisha muda wake ambazo zinaathari kubwa kwa afya ya binadamu kumewezesha kupata zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa mwezi kupitia aparesheni hiyo nchini.

Amesema hivi sasa serikali imekamilisha na kuanza kurekebisha mpango kabambe wa mifugo Tanzania ambao umelenga kuhakikisha afya ya mifugo kwa kuwezesha upatikanaji wa dawa na chanjo za mifugo kwa urahisi ili kufikia soko la kimataifa hasa baada ya kuona mazao mengine ya mifugo hayaruhusiwi kuingia kwenye masoko ya nchi mbalimbali duniani.


Mkurugenzi Mkuu wa ANSAF bwana Audax Rukonge akitoa neno kwa wanahabari (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo.

Pia amesema mpango huo umezingatia swala la kuboresha malisho kwa wafugaji ili kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kuhakikisha swala la uhamilishaji wa mifugo linapewa nafasi ili kupata aina za mifugo inayohitajika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la ANSAF Bwana Audax Rukonge akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo amesema fursa zinaendelea kutokea kila siku lakini watu hawaziangalii na kuzichangamkia.

“Hivi karibuni tunatarajia Afrika kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia na idadi kubwa ya watu watakaokuja watahitaji Nyama, Mayai na Maziwa hivyo lazima tujipange ili wakati huo ukifika na sisi tukauze bidhaa zetu baada ya kukosa fursa kama hiyo mashindano hayo yalipofanyika Afrika ya Kisini” Alisema Rukonge.



Wanahabari wakifuatilia neno la ufunguzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Mifugo na uvuvi.

Mkurugenzi huyo wa ANSAF amesema sekta hiyo inahitaji uwekezaji wa serikali, sekta binafsi na wadau wengine ili iweze kutoa tija inayotakiwa huku akibainisha maeneo ya fursa kuwa ni katika unenepeshaji wa mifugo,Madawa ya mifugo na Chanjo,Uhamilishaji (breeding) pamoja na uzalishaji wa chakula cha mifugo.

Akizungumzia lengo la warsha hiyo ya siku mbili kwa wanahabari hao Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ANSAF Bw. Mbarwa Kivuyo amesema ni kutaka kukumbushana na kuelimishana juu ya changamoto na fursa zilizopo kwenye sekta ya mifugo na kuona namna ya kuzitumia fursa hizo katika kuleta matokeo makubwa.

Post a Comment

0 Comments