SUAMEDIA

SUA KUWA KITOVU CHA UZALISHAJI WA CHAKULA UKANDA WA AFRIKA MASHARIKI NA KATI

Calvin Gwabara
Morogoro
Serikali ya Ufaransa kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania imeahidi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na  wadau wengine katika kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula na malighafi zingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Ufaransa nchi Tanzania Mhe. Fredrick Clavier wakati wa ziara yake chuoni hapo iliyolenga kujifunza kuhusu mradi wa Kilimo Hifadhi unaofadhiliwa na ubalozi wa Ufaransa kwa kushirikiana na  Shirika la Misaada la Switzland  (SWISSAID) na kutekelezwa na timu ya watafiti wa SUA,SAT na TOAM ambapo ubalozi huo umechangia kiasi cha EURO 850,000.



Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Fredrick Clavier akisisitiza jambo katika kikao hicho (Picha na Calvin Gwabara)
“Mradi huu wa miaka mitano unalengo la kuboresha maisha ya wakulima wadogo wapatao elfu 6 na kuhifadhi baioanuai  na mazingira kupitia uzalishaji kwa kutumia kilimo hai, matumizi sahihi ya mnyororo wa thamani wa kilimo hai, kuimarisha vikundi 269 vya wakulima wadogo wadogo, taasisi mwamvuli za vyama hivyo na kuweka kumbukumbu mbinu za kilimo hai zilizokubaliwa na wakulima ili kusaida utetezi  wa kitaifa na kimataifa” Alisema Balozi Fredrick Clavier.
Balozi huyo  ameongeza  kuwa katika mikakati yake anataka kuona kunakuwa na ushirikiano mkubwa kati ya wataalamu wa SUA na kutoka vyuo vingine nchini Ufaransa lakini pia wataalamu na wanafunzi hao waweze kutembeleana pamoja  ili kubadilishana uzoefu.
Amewataka wataalamu wa SUA, FAO, IRD na SWISSAID kukaa pamoja na kuangalia maeneo mawili au matatu ya mashirikiano katika utafiti na  kuandika mradi wa pamoja na kisha kuuwasilisha kwake ili aweze kuuombea fedha kwenye Serikali yake.


Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda akiteta jambo na mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani FAO Bw. Fred Kafeero (Picha na Calvin Gwabara)

Awali akitoa taarifa fupi ya kazi za SUA, Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa Serikali ya Ufaransa ina historia ya muda mrefu na SUA kwani imefadhili baadhi ya miradi hususani mradi wa Kilimo Bustani na ujenzi wa jengo la kufundishia.

“Ujio huu wa Balozi  ni faraja kwa Chuo kwani ni hatua muhimu ya kufungua milango ya ushirikiano zaidi baina ya chuo na Serikali ya Ufaransa katika Nyanja za utafiti na maendeleo katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya tano ambayo inahimiza uwekezaji ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025” Amesema Prof. Chibunda.



Viongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wakiongozwa na Prof. Chibunda aliyevaa miwani mbele wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Ubalozi wa Ufaransa nchini ulioongozwa na Mhe. Balozi Fredrick Clavier aliyekaa katikati mbele na kushoto kwa Balozi ni mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani FAO Bw. Fred Kafeero ( Picha Calvin Gwabara)


Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani FAO Bw. Fred Kafeero  amesema kuwa FAO Tanzania wapo tayari kuingia kwenye ushirikiano huo na kwamba atatuma wataalamu kutoka ofisi yake ili waweze kukaa na timu ya watu watakaoteuliwa kuandaa mradi huo wa ushirikiano.

Nae mwakilishi mkazi wa SWISSAID Tanzania Bw. Blaise Burnier amesema wao wamesaidia wanafunzi wawili wa shahada ya Uzamivu yaani  PhD kwenye utafiti  unaolenga masuala ya kilimo hifadhi wanaosoma SUA.

Post a Comment

0 Comments